July 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kabudi apongeza maboresho ya huduma PSSSF

Na Joyce Kasiki, Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera na Uratibu), Profesa Palamagamba Kabudi, amepongeza maboresho ya utoaji wa huduma yanayofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), akisema yameongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama.

Profesa Kabudi ametoa kauli hiyo Julai 4,2026 baada ya kutembelea banda la PSSSF wakati wa ziara yake katika mabanda mbalimbali yaliyokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,kwenye maonyesho ya Kimataifa ya Biashara jijinibDar Es Salaa  ambapo amekuta taarifa zake za mafao tayari zikiwa zimeandaliwa.

Amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya PSSSF ya kuboresha huduma kwa wanachama kwa kuhakikisha wanaokaribia kustaafu wanapata huduma kwa haraka, kwa usahihi na bila usumbufu.

Waziri huyo pia amewataka watumishi na wananchi kuachana na dhana potofu kwamba watu wengi hufariki muda mfupi baada ya kustaafu, akisisitiza umuhimu wa kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya ajira.

Amesema changamoto kubwa kwa baadhi ya watumishi ni kutokuweka mipango ya maisha ya uzeeni, hali inayowafanya kutegemea fedha za mkupuo kuanzisha shughuli za kiuchumi mara baada ya kustaafu. Amesema mtazamo huo mara nyingi husababisha changamoto za kifedha baada ya muda mfupi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa PSSSF, Haji Khamis, amesema mfuko huo umeendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma ili kuhakikisha wanachama wanalipwa mafao yao kwa wakati na bila ucheleweshaji.

Amesema PSSSF pia inaendelea kutoa elimu kwa wanachama kuhusu umuhimu wa kujiandaa mapema kwa maisha ya kustaafu, akisisitiza kuwa pensheni ya kila mwezi ndiyo msingi wa maisha endelevu ya mstaafu badala ya kutegemea fedha za mkupuo pekee.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kuwasaidia wanachama kupanga matumizi na uwekezaji wao mapema ili wanapostaafu waendelee kuwa na utulivu wa kifedha na maisha bora.