Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tanga
IMEELEZWA kuwa juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali za kuimarisha doria katika maeneo ya mipakani na fukwe za Bahari ya Hindi ,kumesaidia kupunguza vitendo vya uingizaji wa bidhaa za magendo kupitia bandari bubu zilizopo mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian,amezungumza hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yaliofanyika mkoani, aliseme mbali na juhudi hizo pia utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za kodi, forodha na taratibu za biashara halali zimesaidia kupunguza vitendo hivyo.

Dkt.Burian amesema, hatua hizo zimeongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya biashara haramu, huku zikichangia kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya Serikali na kujenga mazingira bora ya ushindani kwa wafanyabiashara wanaozingatia sheria.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya ulinzi na usalama,TRA,mamlaka nyingine za Serikali pamoja na wadau wa sekta ya biashara, ambao wameendelea kushirikiana katika kubaini na kudhibiti njia zinazotumiwa kusafirisha bidhaa za magendo.
Sanjari na hayo amewataka wafanyabiashara kuendelea kuwa wazalendo kwa kulipa kodi stahiki na kuachana na vitendo vya ukwepaji kodi, akisisitiza kuwa mapato yanayokusanywa ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara,shule,vituo vya afya,hospitali pamoja na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga,CPA.Castro John,amesema katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996,imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, hali iliyochangia kuimarika kwa uwezo wa Serikali kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo.
CPA.John amesema,makusanyo ya kodi yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka sh.bilioni 531 mwaka wa fedha 1996/1997 hadi kufikia sh.trilioni 32 mwaka wa fedha 2025/2026,jambo linaloonesha mafanikio ya maboresho yaliyofanywa katika mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi nchini.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa na utekelezaji wa mageuzi mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa katika ukusanyaji wa kodi, kuboreshwa kwa mifumo ya kidijitali, utoaji wa elimu kwa walipa kodi pamoja na kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara nchini.
Ameongeza kuwa TRA itaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia, kupanua wigo na kuboresha huduma kwa walipa kodi pamoja na kuimarisha mazingira rafiki ya ulipaji kodi, hatua ambazo zitasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na maendeleo ya Taifa.
Maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yamekuwa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, huku yakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kujenga mfumo imara wa ukusanyaji mapato kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.


More Stories
Mwaselela awafariji wafanyabiashara walioathiriwa na moto
Waokaji watakiwa kujiunga na ushirika
Zambia yapongeza mafanikio ya Tanzania Sekta ya Umeme