May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jemedari Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za TASWA

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), imemteua Jemedari Said Kazumari kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania zinazotolewa na TASWA.

TASWA imerejesha utoaji wa tuzo zake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na zitaanza tuzo za kila mwezi kuanzia Julai 2023 hadi Juni 2024, kisha itafanyika sherehe ya kuzawadia wanamichezo wote waliofanya vizuri mwaka 2023/24 kwa michezo mbalimbali kadri Kamati ya Utendaji ya TASWA itakavyopanga kwa ushauri wa Kamati ya Tuzo.

Jemedari ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, akiwa pia na leseni B ya ukocha wa mpira wa miguu, ni mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu katika timu mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Mbali na hivyo, pia aliwahi kuwa Meneja wa Leseni za Vilabu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), na Ofisa Maendeleo wa shirikisho hilo kwa miaka minne.

Pia, alikuwa Meneja wa timu ya Azam FC iliyochukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2012/2013, alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF na pia Mjumbe wa Kamati ya Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72). Pia ni mfuatiliaji mzuri wa michezo mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo atakuwa Mbonile Burton, ambaye aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Gofu Wanawake Tanzania (TLGU). Pia ni mtaalam wa michezo ya tenisi, kriketi, skwashi, mpira wa meza, vinyoya na riadha.

Katibu wa kamati hiyo atakuwa Ramadhan Mbwaduke, ambaye alikuwa mwandishi wa habari za michezo kwa zaidi ya miaka 20 akiwa katika ngazi ya uhariri, pia ni mtaalamu wa michezo mbalimbali nchini.

Wajumbe ni Tullo Chambo, Wilson Oruma, Patrick Nyembera, Evance Mhando, Amry Masare, Aaron Mpanduka, Ramadhani Mwelondo, Cosmas Mlekani, Adam Lutta, Gift Macha, Charles Abel, Paschal Kabombe, Mussa Mwakisu.

Wengine ni Anuary Binde, Rahel Pallangyo, Tagato James, Ezekiel Ombopo, Alex Luambano, Faustine Felician, Abisay Stephen Jr, Abdul Mkeyenge, Yusuph Badi, Omary Katanga, Irene Kilango, Athanas Kazige, Suleiman Jongo, Fatma Chikawe na Abdallah Ibrahim.

Dhamira ya TASWA ni kuhakikisha michezo yote inayotambuliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), inafuatiliwa na kwa wale watakaostahili kupewa tuzo wanafikiwa. Uzinduzi wa kamati utafanyika wiki hii.