Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
HAlMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imevuka lengo la uandikishaji darasa la kwanza kwa mwaka 2026,baada ya kuandikisha wanafunzi 14,669 sawa na asilimia 104 ya maoteo yaliyowekwa.
Akizungumza na Timesmajira Online,Ofisa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Mwalimu Mashelo Bahame, alisema mafanikio hayo yametokana na uhamasishaji uliofanywa katika kata na mitaa mbalimbali ili kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto shule.
Amesema halmashauri hiyo iliweka lengo la kuandikisha wanafunzi 14,087 wa darasa la kwanza pamoja na watoto 14,393 wa elimu ya awali kwa muhula wa masomo wa mwaka 2026.
Ambapo oezi la uandikishaji lilianza Desemba 2025 na kuhitimishwa Machi 31, 2026, huku idadi ya wanafunzi waliolengwa kwa darasa la kwanza ikikamilika Februari 28 mwaka huu.
Bahame amesema, halmashauri hiyo ina jumla ya shule za msingi 165, ambapa za Serikali ni 84 na binafsi ni 81 huku shule za Serikali zikiwa na walimu wa kutosha, vitabu na miundombinu rafiki kwa watoto wote wakiwemo wenye ulemavu.
Amesema ufaulu mzuri wa shule za Serikali ambazo baadhi zimekuwa zikipata wastani wa daraja ‘A’, kama shule binafsi katika mitihani ya kitaifa pamoja na halmshauri hiyo kuendelea kuongoza kimkoa kwa miaka minne mfululizo,imeongeza imani kwa wazazi na kufanya mwitikio kuwa mkubwa wa kuandikisha watoto shule ikizingatiwa elimu inatolewa bila malipo.
Bahame amesema,licha ya mafanikio hayo, elimu ya awali ilifanikiwa kuandikisha watoto 12,848 pekee sawa na asilimia 89 ya maoteo, huku asilimia 11 ya watoto waliolengwa kutofikiwa.
Ameeleza kuwa sababu kubwa iliyochangia upungufu huo ni baadhi ya wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi pamoja na vituo vya kulelea watoto mchana maarufu kama “day care”.
Aidha,amesema wazazi wengine hushindwa kuwapeleka watoto katika shule za Serikali kutokana na hofu ya usalama, hasa pale shule inapokuwa mbali na maeneo wanayoishi.
“Wazazi wengi hutoka nyumbani asubuhi kwenda kutafuta kipato na kurejea usiku, hivyo huona ni salama zaidi kuwapeleka watoto wao katika shule za karibu au kusubiri waandikishwe darasa la kwanza,”amesema Bahame.
Mwisho

More Stories
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77