May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Huduma za afya za kibingwa kutolewa bure Tanganyika

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline Tanganyika.

WANANCHI wenye changamoto za kiafya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi wamatakiwa kujitokeza katika hosptali ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupewa matibabu na madaktari bingwa 18 wabobezi kutoka nchini Marekani ambapo huduma mbalimbali za upasuaji utafanyika bure kuanzia Aprili 6 hadi 13 mwaka huu.

Ujio wa madaktari hao kutoka Marekani unatokana na halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kwa kushirikiana na Taasisi ya Norbert and Friends Mission kutambua ukamilifu wa binadamu kimwili,akili na kijamii na kutokuwepo kwa maradhi ni raslimali muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Shaban Juma,wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo ameeleza wakati serikali ikiendelea kupanua huduma za afya kwa kujenga zahanati 14 na vituo vya afya ili kuepusha wagonjwa kusafiri umbali wa km 150 kutafuta huduma za afya za kiwilaya wameona vema kusogeza huduma za kibingwa katika hosptali ya wilaya hiyo.

Juma ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo,wa Mkoa wa Kigoma na Tabora pia wanakaribishwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya kibingwa kwani wasipoweza kutumia fursa hiyo matatibu ya namna hiyo yatawalazimu kusafiri kwenda Hosptali ya Kada ya Rufaa jijini Mbeya, KCMC Moshi, Buganda Mwanza, Benjamin Mkapa Dodoma au Hosptali ya Taifa Muhimbili.

“Huduma za madaktari bingwa ni muhimu ambazo mara chache sana kuzipata kwa sababu ni huduma ambazo huwezi kuzipata kwa gharama nafuu utazipata kwa gharama kubwa lakini hapa sisi tumeona kuzileta hapa ili kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini ambao hawawezi kuzifuata mbali” amesema.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Dkt.Alex Mrema amesema kupitia idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa shirika la Norbert and Friends Missions kupitia tafiti na kubaini kuwepo kwa asilimi 15 ya magonjwa yatokanayo na mtindo maisha waliandika andiko kuweza kupata mradi wa huduma ya afya za kibingwa ambapo huduma za upasuaji wa kibingwa kwa wananchi utafanyika.

Dkt.Mrema amesema kuwa huduma zitakazotolewa na madaktari bingwa kutoka Marekani kwa awamu ya kwanza ni upasuaji wa uso na kichwa ,masikio,pua na koo pamoja na upasuaji wa eneo la tumbo.

Awamu ya pili utakaofanyika kuanzia Mei 4 hadi 11 mwaka huu ni upasuaji mkubwa wa eneo la tumbo kwa watoto na watu wazima ukihusisha upasuaji wa Ngiri ya korodani,eneo la tumboni,uvimbe na saratani ya matiti,Upasuaji wa mfuko wa tumbo wenye uvimbe au saratani,utumbo mwembaba na mpana,upasuaji wa Puru,Ini na upasiaji wa korodani.

Vilevile baadhi ya upasuaji wa tezi kubwa na Koo,Tezi za mdomo,kansa za Koo, Upasuaji wa Kifua ni pamoja na upasuaji wa mapafu,mrija wa chakula,mfuko wa chakula na eneo linalotoa acid, Upasuaji wa mataya na urembo pamoja na upasuaji wa kinamama kwa mama upasuaji wa kuondoa kizazi,upasuaji mfuko wa mayai na mkojo.

Naye,Mkurugenzi wa Shirika la The Norbert and Friends Missions (NFM-BRIGHT),Joel Yalanda amesema kuwa kwa kushirikiana na halmashauri hiyo baada ya kufanya tafiti ya magonjwa ambayo watu yanawasumbua kutokana na mtindo wa maisha ni mengi hivyo kuona umuhimu wa kuandika andiko ili kuwezesha matibabu kwa wagonjwa.

Amesema kuwa wananchi wote wa ndani ya wilaya ya Tanganyika,Mkoa wa Katavi wanakaribishwa kupata huduma hizo za kimbingwa ambapo watalazimika kufanya uchangiaji mdogo sana wa dawa na vipimo.