November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali za rufaa za mikoa zapatiwa mashine za selimundu

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara  ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Prof. Abel Makubi amewataka Waganga Wafawidhi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini kuendeleza kampeni  ya upatikanaji wa vifaa vya kupimia ugonjwa wa Selimundu katika maeneo yao ili kukabiliana na ugonjwa huo.  

Akizungumza leo,Septemba 23,2021 Jijini Dodoma,katika hafla ya kupokea vifaa vya kupimia ugonjwa wa Selimundu zilizotolewa na Taasisi ya General De Pharmacy Limited ya Mkoani Arusha ,Katibu Mkuu huyo amesema  gharama za upatikaji wa mashine za kupimia ugonjwa huo zipo juu ambazo ni shilingi milioni 300 mpaka 400.

“Kama tunavyojua ugonjwa wa Selimundu bado ni tatizo hapa nchini inachangia asilimia 6.7 ya vifo vya Watoto chini ya miaka mitano.Vilevile takwimu zinaonesha asilimia  15 hadi 20 ya watanzania wanavinasaba vya Sikoseli hivyo jitihada zinahitajika ili kusaidia mapambano ya ugonjwa huu.

“Natumani hizi mashine ambazo mnazipata ambazo zitaanzia katika Hospitali za Rufaa zitashuka mpaka chini  zitasaidia kukabiliana na ugonjwa huu,”amesema Prof.Makubi

Hata hivyo,amewaomba  Waganga Wafawidhi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Wilaya kuendeleza kampeni  ya upatikanaji wa vifaa vya kupimia ugonjwa wa Selimundu katika maeneo yao ili kukabiliana na ugonjwa huo.  

“Niwaombe waganga wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Wilaya na Mikoa kutoa sapoti ya hii kampeni ya  hivi vifaa ambavyo vitasaidia kupima mapema  wagonjwa ambao wana  sikoseli,nitoe rai kwa wadau wengine wa maendeleo kuendelea kutoa misaada mbalimbali katika sekta ya afya ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi,”amesema

Prof. Makubi amesema anatamani kuwe na kituo cha kukabiliana na ugonjwa huo hususani Mikoa yenye tatizo hilo  hivyo amewaomba wadau wenye uwezo kusaidia jambo hilo.

“Lakini pia nilikuwa natamani wadau wetu tunahitaji kujenga ‘centre’ ya kukabiliana na ugonjwa wa Sikoseli hapa nchini nipendekeze wadau wenye uwezo basi tushirikiane hususan mikoa ambayo ina tatizo zaidi,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa General de Pharmacy Lmt, Neville Mushi amesema kuwa vifaa walivokabidhi vimegharimu shilingi Millioni 28.

“Lengo la kukabidhi vifaa ni baada ya kusikiliza hotuba nyingi katika maadhimisho ya siku ya Selimundu duniani kuona kuwa tatizo hili ni kubwa sana Nchini,”

“Tulipokea maombi kutoka kwa chama Cha selimundu Tanzania wao walianza kuomba mashine mbili lakini sie kwa namna ya kipekee tulivoguswa tuliamua kuwapatia mashine 5 pamoja na vipimo vya test vya 50 kwa 50,”alisema Mkurugenzi 

Aidha, amesema kuwa kipimo hicho hakitakuwa kikipima selimundu pekee bali kinauwezo wakupima magonjwa mengine pia kama Maralia,HIV pamoja na UVIKO-19.

Naye,Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto ambaye alimwakilisha  Mganga Mkuu wa Serikali,Dkt.James Kihologwe amesema kwa sasa  Serikali ina vituo vitano ambavyo vinapima ugonjwa wa Selimundu hivyo wamejipanga kuhakikisha huduma ya upimaji inakuwa karibu na mwananchi.

Amesema takribani asilimia 6.7 ya vifo vya watoto wachanga vinatokana na ugonjwa wa Selimundu na takribani asilimia 15 mpaka 20 ya watanzania wanavinasaba vya ugonjwa huu na  kila mwaka watoto 11,000 wanazaliwa wakiwa na tatizo la ugonjwa huo.

“Kwa hiyo tunataka huduma hizi zifike karibu na wananchi nini cha kufanya ni kuhakikisha vifaa vinafika hii ni chachu tu kuonesha katika hospitali zetu ni rahisi kuwafikia lengo letu ni kuhakikisha watu wengi zaidi wanapimwa kama wanavinasaba vya ugonjwa wa selimundu,”amesema.