October 20, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lowassa:Rais Samia anaijenga nchi vizuri

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Ngoyai Lowassa (pichani juu kushoto) amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya ya kujenga uchumi wa nchi.

Lowassa ametoa pongezi hizo leo Septemba 24, 2021 kupitia ujumbe maalum aliouandika ukifafanua mambo mbalimbali kuhusiana na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

“Kwanza nianze kwa kumpongeza na kumshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuifanya vyema kazi ya kuijenga nchi na kisha kuendeleza safari ya kujenga uchumi imara.

“Kupitia hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York Marekani jana Alhamisi, Mama Samia amelirejesha tena taifa letu katika ramani ya Dunia.Katika kipindi kifupi alichokuwa madarakani, Rais Samia amefanikiwa kuanza kujenga imani ya sekta binafsi katika kushiriki kwenye ujenzi wa uchumi.

“Safari ambayo hatuna budi sote kumuunga mkono na kumsaidia, ili aliwezeshe taifa kuwa imara zaidi kiuchumi na kuiweka nchi katika utawala wa sheria.Rais Samia amethibitisha pasi na shaka kwamba Tanzania imepata nyota ya jaha kwa kuwa na kiongozi mkuu mwanamke hodari na shupavu ambaye leo hii tuna kila sababu ya kujivunia na kumuunga mkono,”ameeleza kupitia taarifa hiyo.