July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hati miliki 527 zakabidhiwa kwa wananchi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Kwimba

HATI miliki 527 zimekabidhiwa kwa wananchi wa Kijiji cha Solwe wilayani Kwimba mkoani Mwanza, huku Serikali ikisisitiza kuendelea kuimarisha huduma za upimaji wa ardhi na utoaji wa hati hizo ili kuwawezesha kutumia ardhi kama rasilimali ya kukuza uchumi na maendeleo.

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Leonard Akwilapo,akizungumza jJulai 6,2026 wakati wa hafla ya ugawaji hati miliki 527 katika kijiji cha Solwe wilaya ya Kwimba jijini Mwanza,alisema upatikanaji wa hati miliki unawawezesha wananchi kutumia ardhi yao kama dhamana ya kupata mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha, hatua ambayo uchochea uwekezaji, biashara na maendeleo ya familia.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kusisitiza upimaji rasmi wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ili kupunguza na hatimaye kuondoa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikikwamisha maendeleo kwa baadhi ya maeneo.

Hata hivyo amewahamasisha wananchi kuhakikisha wanakuwa na namba za NIDA ili kurahisisha shughuli za upimaji na taratibu za kumilikishwa ardhi huku akikemea viongozi wa vijiji wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuuza ardhi.

“Mwenyekiti siyo mmiliki wa ardhi ya kijiji, ardhi inauzwa kutokana na maamuzi ya wananchi wote kwenye mkutano wa kijiji, viongozi msijichukulie sheria mkononi kuuza ardhi,”amesisitiza Dkt.Akwilapo.

Kwa upande wake Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba,Joshua Majimbe amesema wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 119, ambapo vijiji 97 vina sifa ya kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Amesema kati ya vijiji hivyo, vijiji 24 tayari vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, huku vijiji 22 vikiwa tayari vimetangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali.

Majimbe amesema pamoja na mafanikio hayo, utekelezaji wa shughuli za upimaji na umilikishaji wa ardhi umekuwa ukikabiliwa na changamoto za ufinyu wa bajeti pamoja na upungufu wa watumishi katika Idara ya Ardhi ya Halmashauri hiyo.

Kutokana na hali hiyo,amesema Halmashauri iliingia makubaliano na makampuni binafsi ya upimaji ili kushirikiana kuandaa hati miliki za kimila katika vijiji 15 ambavyo vilipangiwa matumizi ya ardhi mwaka 2023.

Amefafanua kuwa makampuni hayo yaligawiwa maeneo ya utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia makubaliano rasmi (MoU), hatua iliyolenga kuongeza kasi ya upimaji na utoaji wa hati kwa wananchi.

Naye Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza Wilson Luge amesema,Mkoa huo kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri wanaendelea kupanga miji na kuhakikisha maeneo mengi yanapimwa na mipango ya matumizi ya ardhi inaendelea kuandaliwa ili maeneo yote yapimwe.

Hata hivyo Diwani wa Kata ya Wala Elias Kapunda,amemuomba Waziri wa Ardhi kuipa kipaumbele Wilaya ya Kwimba katika kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za upimaji wa maeneo ambayo bado hayajapimwa.