Na Fresha Kinasa,Times Majira Online, Mara.
SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania(HGWT) limesema litaendelea kutekeleza kikamilifu Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji 2025/26 – 2029/30 kwa kutoa elimu kwa wananchi ili kukomesha mila hiyo mkoani Mara.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samwelly, leo Julai 27, 2026 wakati wa zoezi la utoaji elimu na usambazaji wa mkakati huo katika kata za Rung’abure, Nyansurura na Kibanchabancha Wilayani Serengeti.
Rhobi ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa timu inayosambaza Mkakati huo pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, amesema anaamini ukitekelezwa ipasavyo wananchi watapata elimu sahihi kuhusu madhara ya ukeketaji.
“Kupitia elimu hiyo tunaamini mila hii itatokomezwa na wasichana ambao ndio wahanga wakubwa wa ukeketaji watakuwa salama na kuweza kusoma na kutimiza ndoto zao,” amesema Rhobi.
Amefafanua kuwa, lengo kuu la mkakati huo ni kupunguza kiwango cha ukeketaji nchini Tanzania kwa asilimia 50 kutoka asilimia 8 mwaka 2024/2025 hadi asilimia 4 ifikapo 2029/30.

Amesema pia matarajio ya mkakati huo kuwa ni kuhakikisha ifikapo 2030 kuna kupungua kwa ukeketaji, jamii kuachana na mila zenye madhara, utekelezaji mzuri wa sheria, ushirikiano wa kisekta na matumizi bora ya takwimu na tafiti.
“Hivyo taasisi ninayoiongoza itaendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kutoa elimu na kuchukua hatua dhidi ya wanaojihusisha na mila hiyo,” amesema.
Rhoda Samson, mkazi wa Kata ya Rung’abure, amesema mkakati huo ni dira nzuri ya kutokomeza ukeketaji. Amewataka viongozi wa dini na wadau wengine kuendelea kukemea mila hiyo kupitia mafundisho ya kiroho.
Sadick James, mkazi wa Kata ya Kibanchabancha Wilaya ya Serengeti, ameipongeza serikali kwa kuratibu timu hiyo kuwafikia wananchi. Amesema, ukitekelezwa kikamilifu Mkoa wa Mara utaachana na ukeketaji na wasichana wengi wataweza kutimiza ndoto zao.
Awali Suleman Bishagazi, Mhamasishaji kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, amesema mkakati huo umewashirikisha wadau wote na kumpa kila mdau nafasi ya kuwajibika kuhakikisha ukeketaji unakwisha.
Amesisitiza kuwa, kila mwananchi ana wajibu wa kulinda mtoto wa kike na mwanamke dhidi ya ukeketaji kwani ni kinyume na haki za binadamu na sheria za nchi. Hivyo serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kujihusisha na mila hiyo.


More Stories
Alizeti yawa zao kimbilio kwa wakulima Chunya
Askari wanyamapori Babati wapata mafunzo
Mafunzo ya kuongelea kiwango cha kimataifa kutolewa bure Dar