Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Misungwi
WANANCHI wilayani Misungwi mkoani Mwanza wametakiwa kumaliza migogoro ya ardhi na kuzuia kuzalisha migogoro mipya kati vijiji kwa kutumia fursa ya zoezi la upimaji na urasimishaji wa ardhi.
Huku Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikisisitiza kuendelea kuimarisha zoezi la urasimishaji wa ardhi kwa kuwa lina manufaa kwa wananchi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,akizungumza jJulai 6,2026 wakati wa mkutano wa kuhamasisha zoezi la upimaji wa ardhi wilayani Misungwi mkoani Mwanza,ambapo wananchi 668 wa Wilaya hiyo walipatiwa hati miliki ya ardhi,alisema urasimishaji utasaidia kutatua migogoro ya ardhi, kuongeza usalama wa umiliki na kuwapa wananchi uwezo wa kutumia ardhi yao kama rasilimali ya maendeleo.
“Zoezi hili litasaidia sana katika utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi zao kisheria.Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika upimaji wa ardhi na kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa hiyo,”amesema Dkt.Akwilapo.
Dkt.Akwilapo amesema mamlaka za upangaji na usimamizi wa ardhi zitaendelea kupewa kipaumbele katika bajeti za Serikali ili sekta ya ardhi iweze kusonga mbele na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi nchini, Nathaniel Mathew,amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria na matumizi sahihi ya ardhi.
Mathew amesema migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikitokana na ukosefu wa mipaka iliyoainishwa kisheria pamoja na kutokuwepo kwa uelewa wa kutosha kuhusu umiliki wa ardhi.
“Tusizalishe migogoro mipya ya ardhi kati ya vijiji na wananchi.Elimu ya ardhi iendelee kutolewa ili kila mwananchi afahamu haki na wajibu wake,”amesema Mathew.
Naye Mbunge wa Misungwi, Silvery Luboja,amesema zoezi la upimaji wa ardhi ni fursa muhimu kwa maendeleo ya wananchi na kuwataka. Madiwani,Viongozi wa Vijiji pamoja na wataalamu wa ardhi kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu.
Amesema kuwa wananchi wa Tarafa ya Usagara wameonesha utayari wa kupimiwa ardhi zao na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa ardhi huku wataalamu hao kuwa na mkakati mzuri wa upimaji katika maeneo yenye milima na mazingira magumu ili wananchi wote waweze kufikiwa.
Vilevile amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ununuzi wa ardhi ili kuepuka matapeli na migogoro inayotokana na mauziano yasiyo rasmi pamoja na kila mtu kutimiza wajibu wake ili zoezi lifanikiwe n wananchi wanufaike na umilikinrasmu wa ardhi.

More Stories
DC awataka viongozi wa serikali za wanafunzi kulinda amani
Usalama waimarisha Mwanza
Hati miliki 527 zakabidhiwa kwa wananchi