Na Bakari Lulela,TimesMajira Online, Dar
KAMPUNI ya simu ya Halotel na wafanyakazi wake leo wamewatembelea watoto wenye changamoto ya kiafya ya vichwa vikubwa na mgongo wazi pamoja na wazazi/walezi wao waliolazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kusheherekea nao pamoja katika kuadhimisha miaka 6 ya kampuni hiyo na utowaji wa huduma za mwasiliano na kuwaletea mahitaji mbalimbali ya kijamii kama sehemu ya msaada wao kama wafanyakazi.
Mahitaji hayo ambayo ni pamoja na dawa na mahitaji muhimu ya kibinadamu ambayo yatawawezesha watoto hao wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi kuimarisha afya zao pindi wawapo wodini wakisubiri kupatiwa matibabu ambayo ni kwa njia ya upasuaji.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji hayo Naibu Mkurugenzi wa Halotel, Thang Bui Van, akiwa pamoja na Afisa Mahusiano ya nje Halotel Bw. Yassir Matsawily amesema kuwa katika kuhakikisha tunasaidia sekta hii ya afya nchini, tumeona ni vyema kuendeleza fursa hii ya kuja kuwatembelea watoto hawa na kusherehekea nao kwa kuwapa misaada hii ya kijamii ili waweze kuimarika kiafya wanapoendelea kupata matibabu wodini hapa. Hii ni pamoja na kuonesha upendo kwao na kutambua thamani yao katika jamii ya watanzania.
“Tunatambua changamoto mbalimbali ambazo ziko katika kuwapa matibabu watoto wenye matatizo ya kiafya ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wawapo wodini wakisubiri kupata matibabu ya upasuaji hivyo katika kujali na kutambua thamani ya afya zao tumeona ni vyema tukawaletea mahitaji haya muhimu ya kuimarisha afya zao aliongeza Yassir” amesema.
Akiongea baada ya kukabidhiwa msaada huo, kwa niaba ya wazazi wengine wodini hapo bi Rose Vincent amesema, “Tunajisikia furaha sana kukumbukwa na kampuni ya simu Halotel na kupokea msaada huu kutoka kwao, tumefarijika sana na tunaomba waendelee na moyo huu huu wa kuisaidia jamii ya watanzania”
Kwa upande wa Uongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Afisa Uhusiano Bw.Patric Mvungi amesema “Tumefarijika sana kwa kupokea msaada huu kutoka Kampuni ya simu ya Halotel na wafanyakazi wake, tunawashukuru sana kwa kuthamini afya za watoto hawa lakini pia kwa kuunga mkono jitihada za kuisaidia sekta ya afya nchini. Hii ni hatua mpya na kubwa na imekuwa endelevu kwetu sisi katika kuimarisha ushirikiano wetu na Halotel kwa kiwango cha juu hasa katika kuboresha sekta ya afya kwa ujumla”.
Licha ya kampuni ya simu ya Halotel kupiga hatua kubwa katika kusambaza huduma za mawasiliano na kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu nchini nzima, kampuni hii imekuwa ikijihusisha na kutoa misaada mbalimbali kwa jamii ya watanzania.
Hii ni katika kuonesha jinsi inavyothamini na kujali jamii ya watanzania kwa nyanja mbalimbali, ikiwemo kuboresha sekta ya afya na elimu kama moja ya kipaumbele cha kampuni ya hii kwa maendeleo ya watanzania na nchi kwa ujumla.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi