May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hali ya upatikanaji umeme yaimarika ,Megawati 197 zaongezeka

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online ,Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa TANESCO  Gissima Nyamo-Hanga amesema hali ya upatikanaji wa umeme nchini imeimarika huku akisema upungufu wa upatikanaji wa umeme umeshuka kuanzia Septemba Mwishoni mwaka huu  kutoka Megawati 410 hadi kufikia upungufu wa Megawati 213 hivi sasa.

Akizungumza leo Novemba 24 mwaa huu jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchi,Mhandisi Nyamo-Hanga amesema taribani Megawati 197 zimeongezeka katika mfumo wa Gridi ya Taifa ndani ya kipindi cha Septemba hadi hivi sasa kutokana na juhudi  mbalimbali za matengenezo ya mitambo,kuongezeka kwa upatikanaji wa gesi asilia kutoka TPDC sambamba na upatikanaji wa mvua katika ukanda wa vitupo vya kuzalisha umeme vya nyumba ya Mungu.Hale na Pangani.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema,hali ya uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo vya maji bado haijaimarika kutokana na mvua kuchelewa kunyesha katika  mikoa ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji maji katika vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia maji vya Mtera,Kidatu na  Kihansi .

 “Aidha Shirika linautaarifu umma kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya ukanda wa Pwani hususan katika mikoa ya Dar es Salaam ,Pwani na Tanga na zile zinazoendelea kunyesha katika Ukanda wa Ziwa Victoria katika mikoa ya Mara,Mwanza,Simuyu ,Shinyanga,Geita na Kagera ni mvua ambazo kwa ujumla mtiririko wake hauelekei vilipo vyanzo vyetu vya Mtera,Kidatu na Kihansi,

“Na hii ndiyo sababu ya kuendelea  kuwepo na mgao wa umeme pamoja na kwamba mvua zinanyesha katika maeneo ya Kanda hizo mbili.”amesema Mhandisi Nyamo-Hanga

Katika hatua nyingine Mhandisi huyo amesema,mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika Kanda za Pwani na Ziwa Victoria zimeleta athari katika katika miundombinu ya Shirika na hivyo kuongeza makali ya upatikanaji wa huduma ya umeme kwa baadhi ya wateja hasa pale miundombinu inapokuwa imeathirika na mafuriko au kuanguka kutokana na mvua kubwa zinazoambata na upepo au kuharibu barabara  na hivyo kusababisha mafundi kuchelewa kufika.

Aidha amesema,hali ya upatikanaji wa umeme itaendelea kuimarika kutokana na kukamilisha matengenezo ya mitambo iliyokuwa ma hitilafu ,kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia ,kukamilika kwa mradi wa Rusumo utakaozalisha Megawati 27 na Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere utakaozalisha Megawati 2115 .

Mhandisi Nyamo-Hanga amesema ujenzi wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 94.