May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

HakiElimu washauri adhabu chanya kwa wanafunzi mashuleni

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia masuala ya elimu nchini, HakiElimu wamependekeza dhana ya adhabu chanya kupewa mkazo katika mafunzo tarajali na kazini kwa walimu ili kuwasaidia kuepukana na matumizi ya adhabu za kikatili. 

Pia wameiomba serikali kurejea upya mapendekezo yanayotolewa na wadau kuhusu matumizi ya kiswahili kama lugha ya kufundishia ngazi ya sekondari kwani watoto wanaotoka shule za msingi na hasa za umma kuingia kidato cha kwanza wanakuwa hawajawa tayari kuweza kutumia lugha ya kiingereza katika kuzungumza na kujifunza.

Mapendekezo hayo ameyatoa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu tukio la adhabu iliyopelekea kifo cha Mwanafunzi mkoani Mwanza hivi karibuni. 

“Kutumia kiswahili kama lugha ya kufundishia sekondari itatoa fursa kwa watoto kujifunza kwa ufasaha na kufundishwa vema kiingereza na lugha nyingine kama lugha za kigeni hivuo HakiElimu tunaendelea kusisitiza matumizi ya adhabu chanya na vichocheo chanya katika kuimarisha nidhamu na kujifunza”

Ikumbukwe kuwa tukio hilo la Mwanfunzi Gloria Faustine (14) Kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mwinuko, halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mwanza kufariki ilitokana na kuangukiwa jiwe wakati akichimba kifusi kama sehemu ya utekelezaji wa adhabu aliyopewa pamoja na wenzake kwa kosa la kuzungumza lugha ya Kiswahili katika mazingira ya shule.

“Tunafahamu kuwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwezesha kutoa maamuzi yanayozingatia haki, kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, tayari wanamshikilia mkuu wa shule hiyo pamoja na mwalimu wa zamu kama sehemu nya uchunguzi huo”

Aidha Dkt. Kalage amesema wanatambua kuwa walimu wana jukumu la kuwafundisha na kuwajenga wanafunzi katika mwenendo unaofaa ambapo wanaweza kulitekeleza kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo utoaji wa adhabu chanya ambazo zitasaidia kufikia malengo ya utoaji wa adhabu.

“Tunapenda kusisitiza kuwa, adhabu zitolewazo kwa wanafunzi ni lazima zizingatie sana aina ya kosa au tabia inayokusudiwa kurekebishwa, na zilenge katika kumsaidia mtoto kuwa bora zaidi badala ya kumuumiza na kumwongezea hofu”. Amesema Dkt. Kalage. 

Pia amesema kuwaadhibu wanafunzi kwasababu za kitaaluma kama vile kushindwa kuzungumza kiingereza, kuandika au kukokotoa kwenye hisabati hakuwezi kutatuliwa kwa kumpa mwanafunzi adhabu ambayo haimwelekezi katika kujifunza kile anachotakiwa. 

“Katika mazingira haya, mwalimu angeweza kuagiza wanafunzi waandike insha ya lugha ya Kiingereza, kusoma vitabu vingi vya hadithi za Kiingereza na kutoa tafsiri, kutafuta misamiati kadhaa ya kingereza na kuitumia katika sentesi au kuandaa mijadala itakayoendeshwa kwa lugha ya kiingereza na kuhakikisha kila mmoja anashiriki”. 

“Ni muhimu kutambua kuwa huwezi kuimarisha ujifunzaji wa lugha ya pilu kwa kuzuia matumizi ya lugha mama, katika shule nyingi za sekondari kuna kanuni inayosema ; Speak English Only! No English No Service!, Hali hii inatengeneza ombwe kubwa katika ujifunzaji na ufundishaji wa kiingereza au lugha nyingine yoyote).”

Dkt. Kalage amesema Moja ya malengo ya elimu kama yanavyobainishwa kwenye mtaala wa sekondari wa mwaka 2005 toleo la 2013 ni kuwawezesha wanafunzi kuwasiliana kwa ufasaha kwa lugha ya kiswahili pia sera ya elimu ya mwak 2014 inaweka wazi kuwa serikali itahakikisha kuwa lugha ya kiswahili, kiingereza na nyingine za kigeni zinafundishwa kwa ufasaha na ufanisi katika ngazi zote za elimu na mafunzo.