May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Pinda atoa maagizo kwa watumishi wa NHC

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda
ametaka kuwapo mabadiliko makubwa katika nyanja zote za utoaji huduma kwa Watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa ili waweze kuleta tija kubwa kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.

Pia amelitaka shirika la nyumba la Taifa NHC kuhakikisha miradi ambayo inasimamiwa na shirika hilo ikiwemo ujenzi wa ofisi ya Dodoma yenye majengo takribani 10 iende kwa wakati na ijengwe kwa ubora.

Pinda aliyasema hayo jana wakati wa Ziara yake ya siku moja katika shirika hilo, iliyokua na lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa makao makuu kwa niaba ya wafanyakazi wote wa shirika ili kuimarisha taasisi hiyo.

“Nichukue nafasi hii kuwapongezeni kwa kazi kubwa mnazozifanya kawa maendeleo ya Taifa, lakini niwachagize kuwa tunataka mabadiliko makubwa ya utoaji huduma ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa kwa kila mmoja kufanya kazi apaswayo, mpendane, mheshimiane na mthaminiane na sisi kama Serikali tutawaunga mkono kama mlezi wenu,”alisema.

Pinda alisema NHC imefanya vizuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ambayo shirika imesimamia ujenzi wake ikiwemo miji mipya (Safari City- Arusha) , Kuendesha mradi mkubwa jijini Dar es Salaam wa mama samia housing na miradi mingineyo.

Kuhusu ucheleweshwaji wa hati miliki katika maeneo yaliyochukua muda mrefu, Pinda alimuagiza Kamishna wa Ardhi kulifanyia kazi suala hilo.

“Hamuwezi kukwamishana ndani kwa ndani ambapo taasisi hii ipo chini ya wizara yetu , naamini haya yote yatazingatiwa na masuala yanayohitaji marekebisho ya sheria tunaenda kuyaangalia ili tukitoe shirika hapa na tulipeleke mbali zaidi” alisema

Mbali na hayo Pinda Aliutaka uongozi wa Shirika hilo kuutumia ujuzi wa Mkurugenzi Mkuu ambaye ameteuliwa akitokea katika uongozi kwenye taasisi ya sekta binafsi ili Shirika liweze kukua kwa kasi kibiashara kama linavyotakiwa.

“Fanyeni sensa ya kutambua nyumba zenu nchi nzima na mpitie mikataba yenu na wapangaji kuwe na utafiti wa mahitaji ya nyumba maeneo mbalimbali nchini kuna wapangaji wenu wanawapangisha watu wengine kwa fedha nyingi huku wakilipa NHC fedha kidogo, hili siyo jambo jema,”alisema.

Alitaka kuongezwa kasi ya kudai kodi kwa wadaiwa sugu wa Shirika hilo na kwa zile taasisi za Serikali ambazo nazo ni wadaiwa sugu orodha yao iwasilishwe Wizara ya Ardhi ili kusudi Wizara isaidia kudai kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alipendekeza pia uanzishwaji wa vijiji vya mfano vyenye kuleta tija lakini vyenye kuwasaidia Watanzania waliopo pembezoni pamoja na kwamba Shirika linaendeshwa kibiashara .

Alielekeza ushirikishwaji wa Wafanyakazi wote kwa Menejimenti inapoamua kuyabuni mawazo ya maendeleo

“Mimi nataka ustawi wa watumishi pia muwape malengo, watekeleze majukumu yao wanayotakiwa kuyatekeleza, lakini pia wapewe motisha ya kutosha ili kuwa na tija kwa nchi.”