May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso ataka maboresho maslahi ya watumishi,aonya kubaniana

Na Martha Fatael, TimesMajira online

SERIKALI imewaonya baadhi ya maafisa utumishi katika mamlaka za maji nchini na kutaka kuepuka kuonekana ‘Miungu watu’ na kusababisha migogoro isiyo ya lazima jambo linalomlazimu waziri kuingilia kati.

Aidha serikali imetaka Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso,amesema hayo wakati anazindua bodi mpya ya Muwsa na kutaka kutimiza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/25.

Amesema baadhi ya maafisa utumishi wamekuwa sehemu ya unyanyasaji kwa wafanyakazi jambo ambalo linashusha morali ya kufanyakazi kwa bidii.

“Wewe afisa utumishi inatakiwa uwe kimbilio la wafanyakazi, siyo ukiona changamoto ya mtumishi nawe ndiyo unapigilia msumari ili akunyenyekee,hiyo siyo sawa, badilikeni ” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso ametaka Muwsa kupunguza kiwango Cha maji yanayopotea kutoka Kiwango 27.35 hadi kufikia chini ya asilimia 20.

Aweso amesema wizara imekubali maombi ya MUWSA juu ya Ujenzi wa bwawa la maji la Weruweru na inatafuta wafadhili kwa ajili ya bwawa Hilo litakaloongeza huduma maeneo ya Moshi, mji Mdogo wa Bomang’ombe na Hai.

Kuhusu upanuzi wa mabwawa ya maji taka Wizara inatambua umuhimu wa mfumo huo na imetenga fedha kwa ajili ya kuunganisha Kiwanda cha Ngozi.

Aidha Waziri ametaka mamlaka kutoza ankara halali za maji kwa wateja wao na badala yake walipe kulingana na matumizi yao.

Awali mkurugenzi wa MUWSA, Mhandisi Kija Limbe amesema inaendelea kuboresha huduma katika maeneo yote ya manispaa pamoja na wilaya za pembezoni.