July 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GGML kuimarisha ushiriki wa watanzania sekta ya madini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mwanza

KAMPUNI ya uchimbaji madini Geita Gold Mining Limited (GGML) imesema itaendelea kuimarisha ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini kupitia ajira,ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za wazawa pamoja na utoaji wa fursa mbalimbali kwa vijana.

Akizungumza Julai 22,2026 wakati wa kongamano la tano la uzingatiaji wa maudhui ya ndani (Local Content Compliance Forum 2026) linaloendelea jijini Mwanza,Ofisa Rasilimali Watu wa GGML Dominic Marandu amesema,kampuni hiyo imefanikiwa kuhakikisha asilimia 98 ya wafanyakazi wake ni watanzania.

Huku zaidi ya asilimia 80 ya viongozi wa kampuni hiyo ni watanzania,jambo linalodhihirisha maendeleo makubwa katika kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani kushika nafasi za uongozi.

Marandu amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya GGML ya kuwawezesha watanzania kunufaika moja kwa moja na rasilimali za madini kupitia ajira zenye tija.

Pia amesema,wameendelea kushirikisha kampuni za wazawa katika shughuli zao za kila siku huku sehemu kubwa ya manunuzi ya bidhaa na huduma zao hufanywa kupitia kampuni za kitanzania ili kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa nchi.

Ameongeza kuwa GGML inafanya kazi kwa karibu na Tume ya Madini kuhakikisha utoaji wa zabuni unazingatia kanuni za maudhui ya ndani na kwamba changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa ushirikiano.

Aidha, amesema kampuni hiyo imeendelea kutambuliwa kwa mchango wake katika uchumi wa taifa, ikiwemo kutunukiwa tuzo ya Rais kutokana na kuwa miongoni mwa walipakodi wakubwa nchini.

Sanjari na hayo amesema watanzania wanapaswa kuendelea kunufaika na rasilimali za madini kwa kuwa sekta hiyo ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi,ambapo kupitia kampuni hiyo takribani watu 7,000 wamenufaika moja kwa moja na shughuli za mgodi huo, wengi wao wakiwa wazawa.

Hata hivyo GGML imeendelea kutoa fursa za mafunzo kwa vijana kupitia programu mbalimbali za uanagenzi na mafunzo kwa vitendo, ambapo zaidi ya vijana 1,200 wamepata nafasi hizo katika kipindi cha miaka ya karibuni.