Na Joyce Kasiki
MHANDISI Daud Enock kutoka Kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (GASCO), amesema jukumu kuu la kampuni hiyo ni kusimamia, kuendesha na kufanya matengenezo ya miundombinu ya gesi asilia inayomilikiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), sambamba na kushiriki katika ujenzi wa miundombinu mipya ya gesi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la GASCO kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mhandisi Enock alisema kampuni hiyo inasimamia mitambo miwili ya uchakataji wa gesi asilia, ikiwemo mtambo wa Songosongo mkoani Lindi wenye uwezo wa kuchakata futi za ujazo 140 milioni za gesi kwa siku na mtambo wa Madimba mkoani Mtwara wenye uwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 210 kwa siku.
Alieleza kuwa baada ya gesi kuchakatwa na kusafishwa, husafirishwa kupitia bomba kuu hadi Kinyerezi, Dar es Salaam, ambako husambazwa kwa makundi mbalimbali ya watumiaji kupitia mtandao wa usambazaji wa gesi.
“Miongoni mwa wanufaika wa gesi hiyo ni viwanda mbalimbali, mitambo ya kuzalisha umeme, taasisi za umma, majengo ya biashara, mahoteli pamoja na matumizi ya majumbani, hatua inayochochea maendeleo ya uchumi na kupunguza matumizi ya nishati nyingine,” alisema.
Aidha, alisema pamoja na kazi za uendeshaji na matengenezo ya miundombinu iliyopo, GASCO pia hutekeleza miradi mipya ya ujenzi wa miundombinu ya gesi pale inapopata zabuni au mahitaji kutoka kwa wateja.
Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita, kampuni hiyo ilitekeleza miradi sita ya ujenzi wa miundombinu ya gesi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuwaunganishia huduma ya gesi wateja wa biashara na taasisi.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili kampuni hiyo, Mhandisi Enock alisema kwa sasa changamoto zilizopo ni ndogo, zikiwemo baadhi ya taratibu za manunuzi zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya shughuli.
Hata hivyo, alisema GASCO inaendelea kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha huduma za usimamizi, matengenezo na ujenzi wa miundombinu ya gesi zinaendelea kutolewa kwa ufanisi kwa manufaa ya Watanzania.

More Stories
Balozi Omar akoshwa na usimamizi matumizi ya Moduli
Mipango haiwezekani bila Takwimu
NACTVET yaonesha mafanikio Sabasaba kupitia mkondo Amali