April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

FCC yatatua malalamiko 63 robo ya kwanza

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

TUME ya Ushindani (FCC ) imesema ikiwa ni moja ya jukumu lao kutatua malalamiko ya walaji, katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka imeweza kutatua  malalamiko 63 yalishughulikiwa ambapo  Kati ya malalamiko hayo, 45 yalipatiwa ufumbuzi na malalamiko 19 yaliyobaki yapo katika hatua mbalimbali za utatuzi.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo Machi 5,2026 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC),Khadija Ngasongwa,wakati akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana ambapo amesema katika jukumu lingine Tume hiyo inasajiji mikataba mbalimbali kwa mujibu wa sheria ambapo mikataba hiyo hupitiwa ili kuhakikisha inazingatia taratibu na kulinda maslahi ya walaji pamoja na sekta ya kifedha

Ngasongwa amesema katika kipindi hiko FCC ilisajili na kuthibitisha mikataba ishirini na saba (27) inayoandaliwa na upande mmoja (SFCC). 

Huku akijata lengo la kuchambua na kusajili mikataba hiyo ni pamoja na kuondoa masharti kandamizi kwa walaji.
Aidha amesema kuwa Tume ya Ushindani imekuwa ikifanya ushirikiano mkubwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili namna ya kuwalinda walaji hasa katika sekta za kifedha ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi.

‎”Ushirikiano huu  umefanyika  kwa lengo la kuboresha huduma jumuishi za kifedha kupitia mifumo madhubuti ya kushughulikia malalamiko ya wateja ili kuhakikisha wanapata huduma bora,”amesema Ngasongwa.

‎Aidha amebainisha kuwa katika kuboresha huduma kwa wananchi, Tume imefanya ushirikiano na Wakala wa Vipimo pamoja na wadau wengine kufuatilia malalamiko ya watumiaji wa huduma za intaneti ambapo wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia matumizi ya vifurushi vya data.

‎Ambapo amefafanua kuwa tafiti zinafanyika ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha wanazolipia kulingana na huduma wanazotarajia.

‎Pia ameongeza kuwa hatua hizo zinalenga kusaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kuhakikisha ushindani huru na wezeshi unaimarika pamoja na kuimarisha uchumi wa soko.

‎Vilevile amebainisha kuwa katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya mwaka 2050, Tume inalenga kuhakikisha ushindani wa kibiashara unaimarika ili kuongeza nguvu ya ununuzi kwa wananchi na kuchochea mzunguko sahihi wa fedha katika uchumi.

Pamoja  na hayo Ngasongwa amesema FCC imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kuu katika kuwaletea maendeleo watanzania hususan vijana ambapo kwa mwaka 2025/2026 imechangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali takribani shilingi 612,099,999.00 kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea maendeleo watanzania hususan vijana.