June 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

FCC yapongezwa kwa kuimarisha vita dhidi ya bidhaa bandia


SERIKALI imetoa wito kwa wazalishaji, waingizaji bidhaa, wasambazaji, wafanyabiashara, vyombo vya habari, vyombo vya dola, mamlaka za forodha, taasisi za umma, asasi mbalimbali pamoja na wananchi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tume ya Ushindani (FCC) katika kubaini na kudhibiti bidhaa bandia.


Pia imeipongeza FCC kwa kuendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na changamoto ya bidhaa bandia na kuitaka kuendelea kutoa kipaumbele katika mipango ya baadaye ili kuboresha mazingira ya biashara nchini.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani (WACD) 2026.


Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuiunga mkono FCC kupitia maboresho ya sera, sheria na mifumo ili kuhakikisha masoko salama na ushindani wa haki, pamoja na kukabiliana na athari za bidhaa bandia kwa afya ya wananchi na uchumi wa Taifa.


Mapunda amesema FCC inapaswa kupanua matumizi ya teknolojia katika uchunguzi, ufuatiliaji na udhibiti wa bidhaa bandia, hususan katika masoko ya kidijitali na mipaka ya nchi ili kuziba mianya inayotumiwa na wahalifu wa kiuchumi.


Akizungumzia kaulimbiu isemayo, “Linda Maisha na Masoko Dhidi ya Pombe, Vilainishi na Sigara Bandia,” amesema bidhaa bandia zina madhara kwa afya, hupunguza mapato ya Serikali na kudhoofisha biashara halali.


Kamishna wa Tume, Said Tunda, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa FCC, Aggrey Mlimuka, amesema kampeni za elimu kwa umma na mijadala ya kitaalamu imeendelea kuongeza uelewa kuhusu athari za bidhaa bandia kwa afya, uchumi na maendeleo ya biashara halali nchini.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia na kuimarisha ushirikiano wa wadau.