May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yatangaza Bei mpya za mafuta kuanza kutumika kesho

Na zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imetoa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini ikijumlishwa na tozo ya shilingi 100 iliyokuwa imetolewa na Serikali awali kutokana na kupanda kwa bidhaa hizo katika soko la dunia iliyosababishwa na vita vya Urusi na Ukraine,kuanzia kesho.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini hapa leo,Mkurugenzi wa Petroli,Gerad Maganga amesema bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli,Dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la Machi 2 mwaka huu.

Amesema kwa mwezi Aprili mwaka huu bei za rejareja za petroli, Dizeli na mafuta ya Taa zimeongezeka petroli kwa shilingi 321 kwa lita sawa na asilimia 12.65,Dizeli kwa shilingi 289 kwa lita sawa na asilimia 12. 04 na mafuta ya taa kwa shilingi 474 kwa lita sawa na asilimia 21.65,mtawalia.

Kwa bei za jumla amesema Petroli imeongezeka kwa shilingi 320.33 kwa lita sawa na asilimia 13.29,Dizeli kwa 288.50 kwa lita sawa na asilimia 12.69 na mafuta ya Taa kwa shilingi 472.41 kwa lita sawa na asilimia 22.72,mtawalia.

Akizungumzia Mikoa ya Kaskazini ambayo ni Tanga,Kilimanjaro, Arusha na Manyara amesema bei za jumla za mafuta ya petroli,Dizeli na mafuta ya Taa  zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa Machi 2 mwaka huu ambapo bei za rejareja za petroli zimeongezeka kwa shilingi 285 kwa lita sawa na asilimia 11 .12 na Dizeli imeongezeka kwa shilingi 295 kwa lita sawa na asilimia 11.90,mtawalia.

Kwa bei za jumla ikilinganishwa na mwezi uliopita bei za petroli zimeongezeka kwa shilingi 284.22 kwa lita sawa na asilimia 11.68 na dizeli kwa shilingi 294.66 kwa lita sawa na asilimia 12.52,mtawalia.

“Kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye matanki ya kuhifadhia yaliyopo Tanga ,waendeshaji wa vituo vya mafuta ya taa katika Mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika Bandaribya Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam  na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika,”amesema.

Aidha amesema kuwa Bandari ya Mtwara imepokea mafuta ya dizeli tu hivyo kwa mwezi huu kwa bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli kwa Mikoa ya kusini ambayo ni Mtwara,Lindi na Ruvuma zitakuwa  sawa na zile zilizotangazwa Machi mwaka huu .

“Kwa upande wa Dizeli kwa Mwezi Aprili mwaka huu bei za rejareja na jumla zimeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita ambapo bei rejareja ya dizeli imeongezeka kwa shilingi 281 kwa lita sawa na asilimia 11.12 huku bei ya jumla ikiongezeka kwa shilingi 279.99 kwa lita sawa na asilimia 11.67,”amesema.