Na Joyce Kasiki,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi kupitia banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Akizungumza katika maonesho hayo , Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa EWURA, David Mwakalosi, alisema mamlaka hiyo ina jukumu la kudhibiti sekta ndogo za nishati kwa kuhakikisha huduma zinapatikana kwa usalama, ubora na kwa kuwalinda watumiaji, huku ikiendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ili kulinda afya za wananchi na mazingira.
Mwakalosi alisema matumizi ya kuni na mkaa yanaendelea kuchangia ukataji wa miti na uchafuzi wa hewa, hali inayoongeza athari za mabadiliko ya tabianchi na magonjwa ya mfumo wa upumuaji. Aliongeza kuwa miti mingi inayokatwa kwa ajili ya mkaa huchukua miaka saba hadi 10 kukua, hivyo matumizi ya nishati safi ni njia muhimu ya kuhifadhi mazingira.
Alisema matumizi ya gesi, umeme na majiko banifu yana faida kubwa ikiwemo kuokoa muda, kupunguza matumizi ya fedha kwa muda mrefu na kumpa mtumiaji uwezo wa kudhibiti kiwango cha joto wakati wa kupika, tofauti na mkaa ambao husababisha upotevu wa nishati na muda.
Aidha, Mwakalosi alionya kuhusu matumizi yasiyo salama ya mkaa ndani ya nyumba, akisema baadhi ya wananchi wamepoteza maisha kutokana na kuvuta hewa yenye sumu ya monoksidi kaboni, hususan katika maeneo ya baridi ambako mkaa hutumika kujipasha joto ndani ya nyumba zisizo na mzunguko mzuri wa hewa.
Aliwahimiza wananchi kutembelea banda la EWURA ili kupata elimu kuhusu teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia, ikiwemo majiko ya umeme yenye matumizi madogo ya nishati .
Mwakalosi alisisitiza kuwa kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia siyo anasa bali ni uwekezaji unaolinda afya, unaookoa gharama na unachangia uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
,

More Stories
Diamond: Usimamizi wa sheria waongeza uwekezaji sekta ya habari
JAB yazindua mwongozo wa Ithibati ya maisha kwa Waandishi Wakongwe
Wananchi wahimizwa matumizi bidhaa za asili kulinda mazingira