May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisa Tarafa ya Ibindo Wilayani Kwimba Jeremiah John

Elimu zaidi inahitajika kukomesha ndoa za utotoni

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

HAKIKA upatapo nafasi ya kumsaidia mwanadamu mwenzio fanya hivyo kulingana na nafasi ulionayo kwani uwezi jua unayemsaidia sasa anaweza kuja kuwa na mchango mkubwa kwako au kwa taifa hapo baadae.

Hivyo ni wajibu wa kila kiongozi na mtu yoyote kutumia nafasi yake katika kuwakomboa wananchi hususani watoto wadogo wanaokumbwa na vitendo mbalimbali vya ukatili ukiwemo wa kingono ambao umegawanyika katika nyanja mbalimbali kama vile kuozeshwa katika umri mdogo, kubakwa, kulawitiwa, kushawishiwa kujiingiza katika masuala ya mapenzi ambayo hupelekea kupoteza ndoto zao na kupelekea kuwa na kizazi hususani cha kike ambacho hakijapata elimu jambo linalochangia kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Katika kulitambua hilo na umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga alitumia nafasi yake ya uongozi katika Wilaya hiyo na akiwa kama mama kuweza kumnusuru binti wa miaka 13 ambaye mwaka jana alikuwa kidato cha kwanza kuolewa baada ya wazazi wake kuwa na tamaa ya kupata mali (Ng’ombe).

Mkuu huyo wa Wilaya hiyo alifanikiwa kumnusuru binti hiyo kuolewa baada ya kuingilia kati na kufanikisha kusitisha zoezi hilo ambalo lilirejesha matumaini kwa mwanafunzi huyo ambaye kwa sasa yupo kidato cha pili katika shule ya Sekondari Tallo iliyopo kijiji cha Mwankuba Wilayani humo.

Akisimulia tukio hilo Ngaga anasema, binti huyo ambaye jina lake limehifadhiwa alitaka kuozwa kutokana na tamaa ya baba yake ya kuhitaji ng’ombe hali ambayo inashangaza katika dunia ya sasa ya mtu kutamani mali zaidi kuliko kumrithisha mtoto elimu ambayo ndio dira na ufunguo wa maisha ya sasa na baadae.

Anasema, alipopata fununu za kuozeshwa binti huyo kinyume na sheria alilazimika kuwakamata wazazi kitu ambacho kilisaidia hadi sasa mtoto huyo anaendelea na masomo yake na hiyo yote inatokana na changamoto ya jamii kutokuwa na uelewa huku koo za huko kupenda kumiliki ng’ombe zaidi.

“Mtoto huyu anapenda kusoma na ndio maana alitoa taarifa baada ya kuona harakati za kuozeshwa, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama tulifanikiwa kumnusuru na sasa anaendelea na masomo yake vyema huku hatua za kisheria zikiendea ambapo kesi hiyo ipo mahakamani kwa sasa,” anasema Ngaga.

Baba mzazi wa binti huyo ambaye ni mtoto wa 13 kati hya 14 alionao baada ya kutembelewa nyumbani kwake na gazeti hili anasema, ni kweli tukio la kutaka kumuozesha binti yake lilikuwepo lakini kwa sasa halitatokea tena na amejikita kumpa elimu anayostahili na asome mpaka atakapoishia mwenyewe kwani akifanya hivyo anaweza kukamatwa.

“Kwa sasa binti yangu yupo kidato cha pili, anaendelea vizuri na masomo yake siwezi kabisa kumuozesh. Kwa vile baba yake nipo lazima atasoma tu lakini akishindwa ataolewa akifaulu ataendelea na elimu ya juu zaidi ili afikie malengo, nimeondoa ubaguzi wa kijinsia kwa watoto wa kike baada ya kupatiwa mafunzo na Mkuu wetu wa Wilaya ambaye anawapigania watoto wa kike sijua kwa vile na yeye ni mama au vipi?,” anasema baba huyo.

Mongo Mbombile ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyambiti anasema, matukio ya kuwaozesha watoto yanayochangiwa na wazazi kupenda mifugo kuliko elimu ambayo ndio msingi wa maisha.

Anasema, wazazi wamekuwa na tabia ya kuomba uhamisho kwa ajili ya mtoto wake kuhama shule moja kwenda nyingine lakini inakuwa siyo kweli bali anataka kwenda kumuozesha tu.

“Usifikirie kuwa ukimpa mtoto uhamisho ataenda kusoma, hiyo ni mbinu wanayotumia kwenda kumuoza ili wasiweze kushtukia,sasa Kuna utaratibu mpya wa watoto wanaohamishwa wengi wakielekea Mpanda hasa wa kike hao wanaenda kuolewa tunamshukuru sana Mkuu wa Wilaya alilisimamia hilo la mtoto kutaka kuolewa na kumnusuru katika adha hiyo,”anasema Mombile.

Ofisa Tarafa ya Ibindo, Jeremiah John anasema, tatizo lililopo ni kuwa wazazi wengi hawajui umuhimu wa mtoto hivyo jukumu walilo nalo ni kuwakamata wazazi, ndugu na marafiki wataohudhuria siku ya utoaji wa mahali kwa mtoto ambaye ni mwanafunzi na kuwafikisha kwenye vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake .

“Hivi karibuni kuna binti alifaulu kuingia kidato cha kwanza lakini tayari baba yake alikuwa ameshachukua mahali na tuliingilia kati. Pia kuna mwingine walikuwa ndio wanapokea mahali tuliwasomba watu wote waliokuwa eneo la tukio hiyo pia ilisaidia kwani sasa matukio yameanza kupungua” alieleza John.

Aliongeza kuwa, kwa kushirikiana na ngazi mbalimbali ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Wilaya na vyombo vya usalama wanafanya ufuatiliaji sana ambao umesaidia kujenga hofu kwa jamii na kuachana na matendo hayo .

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Ngudu Wilayani Kwimba, Mathias Kadinda, anasema wazazi na jamii ya Kwimba kwa ujmla inapaswa kujikita katika kuwekeza kwenye elimu kwa ajili ya watoto wa jinsi zote za kike na kiume bila kufanya ubaguzi na kuacha kuwaozesha watoto kisa ng’ombe ambazo zinatafutwa.

Anasema, wao kama viongozi wa dini mchango wao katika jamii wanakutana pamoja na kujadili hasa namna ya kutokomeza na kupinga ukatili wa kijinsia kama vile wa kingono,uchumi na kiimani.

“Wito wangu kwa wazazi na jamii ya Kwimba wawekeze katika kuwapatia elimu watoto wote,kwani urithi wa elimu ni zaidi ya ng’ombe,wanapowekeza kwenye upande wa elimu itamsaidia mtoto baadae pale atakapoa za kujitegemea kwani atakuwa amerithi kitu cha kudumu,”.

“Siyo kuacha kumsomesha mtoto na kusema ataolewa ili nipate ng’ombe sawa kwani tutambue kuwa thamani yake haitolingana na ile ambayo utamsomesha na akapata elimu ambayo ni urithi wa kudumu ambayo itamsaidia yeye, familia, jamii kwa ujumla na Serikali kwa sababu akisoma anaweza kuwa daktari, muuguzi au kiongozi yoyote ambaye kulingana na utendaji kazi wake akawa na mchango mkubwa kwa Taifa,” anasema Mchungaji Kadinda.