May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EFTA kukopesha vijana kuku bila dhamana

Mkurugenzi wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay akiwakabidhi, baadhi ya wanafufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku ambao kampuni hiyo imevitoa kwa wafugaji mbalimbali bila dhamana. Jumla ya vifaranga 30,000/= vimekabidhiwa kwa wafugaji wa kuku wapatao thelathini katika mikoa mbalimbali hapa nchini. 

Bi Mwanamvua Ngocho, Meneja Masoko wa Kampuni ya Silverlands Tanzania Ltd, wazalishaji wa vifaranga bora vya kuku ambao wanahusika na kuzalisha vifaranga vinavyotolewa kwa mkopo na EFTA kwa wakulima mbalimbali nchini, akimuongoza mkurugenzi mtendaji wa EFTA, kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa vifaranga hivyo.

Mkurugenzi wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay akiwakabidhi, baadhi ya wanafufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku ambao kampuni hiyo imevitoa kwa wafugaji mbalimbali bila dhamana. Jumla ya vifaranga 30,000/= vimekabidhiwa kwa wafugaji wa kuku wapatao thelathini katika mikoa mbalimbali hapa nchini. 

Baadhi ya wanufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku kutoka EFTA, wakiwa katika picha ya pamoja na mkurugenzi mtendaji wa EFTA Bwana Nicomed Bohay, baadhi ya maafisa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha, wakati wa hafla ya kuzindua utoaji wa mikopo ya kuku kwa wafugaji nchini. Picha na mpiga picha wetu.

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online Arusha, Tanzania

Taasisi ya EFTA inayojishughulisha na utoaji wa mikopo ya mashine na magari bila dhamana kwa wajasiriamali na wakulima nchini, imetenga Zaidi ya shilingi Bilioni 3.5 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa lengo la kuwawezesha vijana na wanawake nchini kupata mikopo ya vifaranga vya kuku, chakula Pamoja na mahitaji mengine muhimu ya ufugaji wa kuku bila dhamana.

 Mpango wa mkopo wa vifaranga vya kuku kwa wakulima na hususani vijana na wanawake wasiokuwa na ajira au wanaotaka kujipatia kipato cha ziada ni wa kwanza na wa aina yake kwa taasisi ya kifedha nchini kuutoa  kwa wakopaji.

EFTA imezindua mpango huu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dr Samia Suluhu Hasan, ambaye amekuwa akijipambanua katika kuhakikisha kuwa watanzania na hususani vijana na wanawake wanawezeshwa kiuchumi kwa kuwawezesha kupata mikopo ya aina mbalimbali ambayo itawasaidia kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

 Kwa muda sasa kundi la vijana na wanawake nchini Tanzania, ni miongoni mwa makundi ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira rasmi hatua ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa umasikini miongoni mwa kundi hili.

 Serikali kupitia mpango wa Jenga Kesho Bora unaojulikana kama “Built Better Tomorrow – Youth initiative for Agribusiness (BBT-YIA), umewezesha vijana wengi nchini kupata fursa ya mafunzo na mikopo ya kuanzisha na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji hapa nchini.

 Kampuni ya EFTA katika kuunga mkono jitihada hizo za serikali nayo imeamua kuanzisha mpango wa majaribio wa mkopo wa kuku kwa vijana na wanawake bila dhamana. Hatua ambayo itawezesha makundi haya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji kupitia uwezeshwaji wa mkopo huu bila dhamana, hatua ambayo itakuwa imeondoa ile kadhia ya vijana na wanawake kutokukopesheka katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa kukosa dhamana.

 Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay wakati alipokuwa akiutambulisha mpango huu wa mkopo wa Kuku kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, katika hafla iliyofanyika katika kiwanda ya kuzalisha kuku cha Silverland kilichoko USA-River jijini Arusha.

 Bohay amesema, mpango huu wa mkopo wa kuku kwa vijana na wanawake bila dhamana pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali lakini unakwenda sambamba na malengo ya uanzishwaji wa taasisi yake wa kuwawezesha wajisiriamali na wakulima na hususani kutoka katika makundi hayo kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo ya EFTA inayotolewa bila dhamana.

“Vijana na wanawake wengi hawakopesheki katika taasisi zetu za kifedha kwa sababu wengi wao hawana dhamana ya kuwawezesha kupata mikopo hiyo, ndio maana sisi baada ya kuiona changamoto hii, tuliamua kuja na mpango wa kuwakopesha vifaranga vya kuku bila dhamana, Na tumechagua kuku kwa sababu uwekezaji wake ni wa muda mfupi na mkopaji ndani ya miezi michache anaanza kuona matunda ya uwekezaji wake”

 “Kwa mfano kwa kuku hawa tunaowakopesha wakopaji wataweza kuanza kuwauza baada ya siku sitini, hii ni aina ya uwekezaji ambao unaweza kuona matunda yake ndani ya muda mfupi na ndio maana tunawahimiza vijana wengi na wanawake wajitokeze kuchangamkia fursa hii”  amesema Bohay.

 Bohay ameongeza kuwa katika mwaka wa kwanza wa mpango huu EFTA inategemea kutoa mkopo wa kuku 250,000 nchi nzima, ambapo mpaka sasa wamekwisha kabidhi zaidi ya Kuku 30,000 kwa wafugaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.

 “Tayari tumeanza mafunzo kwa wafugaji walio tayari kukopa na kwa waliohitimu mafunzo tayari tumeisha wakabidhi katika awamu ya kwanza ambayo wafugaji takribani 30, wamenufaika kwa kupata mkopo wa kuku zaidi 30,000. Hivyo niwahimize vijana wengi zaidi wajitokeze mikopo hii ni kwa ajili yako” Amesisitiza Bohay

 Kwa kushirikiana na wazalishaji wa vifaranga vya kuku kama vile Silverland Ltd, na wengine EFTA itamwezesha mkopaji kupata mahitaji yote muhimu kama vile chakula, madawa na vifaa mbalimbali kama mkopo kwa wakati wote mpaka atakapokuwa tayari kuwapeleka kuku wake sokoni.

 Kwa upande wake Meneja Masoko wa Silverlands Ltd, Bi.Mwanamvua Ngocho, ambao ni mojawapo wa wazalishaji wa vifaranga vya kuku ambao EFTA itashirikiana nao katika mpango huu kuhakikisha wafugaji wanapata vifaranga bora, chakula na chanjo ili kumhakikishia mfugaji anapata matokeo chanya kwa wakati.

 “Hapo awali, wateja wetu walikuwa wafugaji wenye uzoefu na mitaji mikubwa. Lakini sasa, kwa ujio wa EFTA, fursa zaidi kwa vijana na wanawake zitafunguka, na sisi kwa kweli tuko tayari kuhakikisha kwanza tunatoa mafunzo makini ya namna ya kufuga kisasa, lakini pia kuzalisha vifaranga vya kuku vyenye ubora zaidi,” alibainisha Ngocho.

 “Tunatamani kuona watu wetu wanaimarika kiuchumi kwa kuwa wafugaji wa kuku, lakini pia afya ya jamii yetu ikiimarika zaidi kwa kula nyama na mayai ya kuku bora kutoka kwa wafugaji wetu, Na hii sasa ndio fursa ambayo naamini hakuna kijana wala mwanamke anaehitaji kujiajiri ataiacha impite” ameongeza Ngocho

 Kwa upande wake kaimu katibu tawala msaidizi mkoa wa Arusha anaeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Bwana Daniel Loroku, ameishukuru taasisi ya EFTA na kampuni ya Silverland kwa kuja na mpango huu wa kusaidia vijana na wanawake kupitia mikopo ya vifaranga vya kuku bila dhamana.

 “Jukumu la serikali ni kuona kila mmoja wetu wetu anashiriki katika ujenzi wa taifa kwa kuchangia pato kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi tunazozifanya, hata hivyo changamoto ya mitaji kwa baadhi ya watanzania imekuwa ni kikwazo cha wao kuwa sehemu ya wachangiaji wa pato la Taifa” Amesema Bwana Loroku.

 “Ujio wa EFTA na aina hii mpya ya mkopo wa vifaranga vya kuku bila dhamana, kwa kweli kwetu kama serikali ni fursa muhimu sana maana itasaidia kuwezesha kundi hili la vijana na wanawake kuweza kujikwamua kiuchumi maana sasa wataweza kuwa na shughuli za kufanya na ambazo zitawapatia kipato ndani ya muda mfupi” Ameongeza Bwana Loroku

 Kwa upande wake Flora Danford Sando, mmoja wa wanufaika wa mpango huu, anaelezea namna ambayo fursa hii itakavyomsaidia katika kuyabadili Maisha yake na hasa baada ya kutafuta ajira kwa muda mrefu bila mafanikio.

 “Baada ya kuhitimu masomo yangu, nilitafuta ajira, lakini kwa Bahati mbaya sikufanikiwa kupata kazi. Nilijaribu pia kutafuta mikopo katika mabenki ili nianze biashara lakini huko nako sikufanikiwa maana nilitakiwa kuwa na dhamana, Nikiwa katika hali ya kukata tamaa ndio nikapata Habari za uwepo wa mkopo huu kutoka EFTA bila dhamana” Anasimulia Sando

 “Haraka sana niliwatembelea EFTA na wakanielezea taratibu zao ambazo nilizifuata, na baada yapo walinipeleka Iringa katika Chuo cha Ufugaji wa Kuku cha Silverlands, ambapo nilipata elimu ya namna bora ya kufuga kuku kisasa, Na leo Nimekabidhiwa rasmi vifaranga zaidi ya miatano ambavyo nitavifuga kwa siku 60, na kisha nitaviingiza sokoni, ambapo baada ya kuuza ndio nitakuja kulipa mkopo wangu” anaeleza Frola kwa furaha.

 Mpango huu wa mkopo kwa wafugaji wa kuku nchini utakuwa ni sehemu ya mwarobaini wa changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake maana utatoa fursa nyingi kwa vijana kujiajiri na hivyo kuwafanya vijana wengi kuwa sehemu ya wachangiaji katika uchumi wa Taifa.