Na Mwandishi wetu,Timesmajira
NCHI Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimejizatiti kuimarisha mifumo ya elimu, kuboresha matokeo ya ujifunzaji na kuongeza uwekezaji katika walimu, ujuzi na usawa wa upatikanaji wa elimu.
Ahadi hiyo imetolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kikanda wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaofanyika jijini Nairobi, Kenya, Katibu wa Baraza la Mawaziri anayeshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maeneo Kame na Nusu Kame nchini Kenya, aliyemwakilisha Rais wa Kenya,Beatrice Moe, alitoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika mafunzo ya walimu, maendeleo yao kitaaluma na kuboresha mazingira ya kazi.
Amesema kadiri ushirikiano wa kikanda unavyozidi kuimarika, mifumo ya elimu katika nchi wanachama inapaswa kuwa na uhusiano mzuri zaidi ili wanafunzi wanaohama kutoka nchi moja kwenda nyingine wasikatishwe masomo kwa sababu ya kuvuka mipaka.
Aidha,ameitaka EAC kujenga mifumo ya elimu inayozingatia usawa na kuwezesha wanafunzi kupata fursa za kusoma katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.

Amesisitiza kuwa mabadiliko ya mitaala hayawezi kufanikiwa bila kuwapo kwa mabadiliko katika ualimu, akieleza kuwa walimu wanapaswa kuonekana siyo tu kama waajiriwa wa mifumo ya kitaifa, bali kama wataalamu wa elimu wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC,Rt.Rebecca Kadaga, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayeshughulikia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Uganda,ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na kuoanisha mifumo ya elimu.

Kadaga amesema elimu inapaswa kuunga mkono ajenda ya kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na kuwaandaa wanafunzi kushiriki katika uchumi wa kikanda unaozidi kuunganishwa.
Amesisitiza umuhimu wa kuoanisha sera za elimu, mitaala na sifa za kitaaluma ili kurahisisha uhamaji wa wanafunzi na wataalamu miongoni mwa nchi wanachama, huku mifumo ya elimu ikizingatia vipaumbele vya pamoja vya maendeleo ya kikanda.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na Kijamii, Hon. Ariik Malueth, amesema Jumuiya hiyo imepiga hatua katika kuanzisha mifumo ya kikanda inayosaidia nchi wanachama kuendeleza elimu kwa pamoja.

Amesema katika ngazi ya elimu ya msingi, EAC imeandaa mikakati ya kusaidia uoanifu wa mifumo ya elimu na kuimarisha msingi wa ujifunzaji wa maisha yote pamoja na maendeleo ya ujuzi.
Kwa upande wa elimu na mafunzo ya ufundi na stadi (TVET),amesema EAC imeandaa Mfumo wa Sifa za Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa EAC, ambao unasubiri kuidhinishwa. Mfumo huo unatarajiwa kusaidia kutambua sifa za kitaaluma, kurahisisha uhamaji wa wataalamu na kuoanisha mafunzo na mahitaji ya soko la ajira la kikanda.
Aidha, Malueth amesema EAC inaendelea kuandaa miongozo ya ukusanyaji wa takwimu za elimu ili kuongeza upatikanaji wa taarifa zinazoweza kulinganishwa na kuaminika kwa ajili ya kutengeneza sera za elimu za kikanda.
Amesema mpango huo pia umesaidia kupitia upya mtaala wa shule za msingi ili kujumuisha somo la Takwimu, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa uchambuzi wa wanafunzi tangu wakiwa
Aidha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Prof. Adolf Mkenda, ametoa wito wa kuwekwa mkazo zaidi katika ujifunzaji wa msingi kama nguzo ya kuboresha matokeo ya elimu.
Prof. Mkenda pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika walimu, elimu bora na maendeleo ya ujuzi, akieleza kuwa mifumo ya elimu inapaswa kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa, uwezo na uwezo wa kuendana na mabadiliko katika ulimwengu wa kazi.
Pamoja na nchi wanachama kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na kutekeleza mageuzi mbalimbali, changamoto za usawa bado zinaathiri watoto katika maeneo ya vijijini na jamii zilizotengwa, wanafunzi wenye ulemavu pamoja na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.

More Stories
Yas yamwezesha mtangazaji kuripoti matukio Mlima Kilimanjaro
Tume zaunganisha nguvu kuimarisha miradi ya maendeleo
Mkenda aitaka EAC kuongeza uwekezaji Sekta ya Elimu