July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia aitangaza Sabasaba kama nguzo ya Biashara,Uwekezaji

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi kwa kipindi cha miaka 50, yakichangia kukuza uzalishaji, biashara, uwekezaji, ajira na kuunganisha Tanzania na masoko ya dunia.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo, Rais Samia alisema maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya Sabasaba si kumbukumbu ya historia pekee, bali ni ushuhuda wa mchango mkubwa wa sekta binafsi, wafanyabiashara, vijana na wajasiriamali katika kukuza uchumi wa taifa.

Amesema maonesho hayo yameendelea kuwa daraja muhimu linalowaunganisha wazalishaji na walaji, wafanyabiashara na masoko pamoja na wawekezaji na fursa mbalimbali za biashara ndani na nje ya nchi.

“Tunapoadhimisha miaka 50 ya maonesho haya, tunalenga kulinda historia yake na kuthibitisha kuwa haibaki kwenye kumbukumbu pekee, bali inatafsiriwa katika kukuza uzalishaji, biashara, uwekezaji, ajira, usafirishaji na kuimarisha ustawi wa watu wetu,” amesema Rais Samia.

Amebainisha kuwa kupitia Sabasaba, wafanyabiashara wadogo wamekua na kuwa wafanyabiashara wakubwa, huku wakulima, wajasiriamali na wabunifu wakipata masoko mapya, mitaji na washirika wa biashara waliowawezesha kupanua shughuli zao.

Rais Samia pia ameeleza historia yake binafsi katika maonesho hayo, akisema aliwahi kushiriki kama afisa wa kawaida na baadaye kusimamia mabanda ya biashara, jambo linalodhihirisha nafasi muhimu ya Sabasaba katika kukuza vipaji na fursa za maendeleo.

“Nimefurahi kuona baadhi ya waonyeshaji ambao walikuwepo tangu nilipokuwa afisa wa kawaida bado wanaendelea kushiriki hadi leo, huku biashara zao zikiendelea kukua,” amesema.

Aidha, amesema maonesho ya mwaka huu yamevutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania, hali inayoonesha kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Amesema ushiriki wa mataifa mbalimbali, ikiwemo Indonesia, unaonesha kuwa Tanzania inaendelea kuaminika kama kituo muhimu cha biashara, uwekezaji na lango la kufikia masoko ya Afrika Mashariki, SADC na Bara la Afrika kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewapongeza viongozi na watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, sekta binafsi, wadhamini, washirika na wadau wote waliochangia mafanikio ya maonesho hayo kwa kipindi cha nusu karne.

Pia ameipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa maboresho ya miundombinu, matumizi ya teknolojia na uendeshaji wa maonesho hayo, akisisitiza umuhimu wa kuyaendeleza ili yafikie viwango vikubwa zaidi vya kimataifa.

“Tuendelee kujitolea kwa nguvu zaidi ili kuyawezesha maonesho haya kufikia hatua kubwa zaidi na kuwa miongoni mwa maonesho yanayotambulika duniani,” amesema.

Chapo Aipongeza Tanzania

Kwa upande wake, Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, amempongeza Rais Samia na Watanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya Maonesho ya Sabasaba, akisema mafanikio hayo yanaashiria miaka 50 ya dhamira ya Tanzania katika kukuza biashara, viwanda, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.

Amesema Sabasaba imekua kutoka maonesho ya kawaida na kuwa moja ya majukwaa muhimu zaidi Afrika katika kukuza biashara, ubunifu, viwanda na uwekezaji.

Chapo amesema kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu inayohusu mageuzi ya viwanda, ubunifu wa teknolojia, uunganishaji wa mifumo ya usafirishaji na kurahisisha biashara za mipakani inaakisi vipaumbele muhimu kwa Afrika katika kujenga uchumi imara na shindani.

Ameeeleza kuwa Tanzania na Msumbiji zimeunganishwa kwanza na historia kabla ya kuwa washirika wa kiuchumi, akibainisha mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa taifa hilo.

“Kabla ya kuzungumzia njia za usafirishaji na minyororo ya thamani katika biashara, watu wetu tayari walikuwa wakitembea pamoja bega kwa bega wakitetea uhuru, ukombozi na heshima ya Waafrika chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na Eduardo Mondlane,” amesema.

Chapo amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee katika mioyo ya wananchi wa Msumbiji kutokana na mchango wake mkubwa katika kupigania uhuru wa taifa hilo.

“Uhuru wa Msumbiji una alama za Tanzania. Wananchi wa Msumbiji hawatasahau kuwa wakati uhuru ulikuwa bado ndoto, Tanzania ilisaidia kuigeuza ndoto hiyo kuwa uhalisia,” amesema.

Kapinga: Miaka 50 Ijayo Tutaongozwa na Mahitaji ya Soko

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Judith Kapinga, amwsema kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita TanTrade imekuwa daraja muhimu la kuitangaza Tanzania katika masoko ya dunia kupitia bidhaa, huduma na fursa za uwekezaji.

Amesema katika miaka 50 ijayo, mkazo utawekwa katika kutafuta masoko kabla ya uzalishaji kufanyika ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi mahitaji ya soko.

“Miaka 50 iliyopita TanTrade ilianzishwa kwa lengo la kuitangaza Tanzania, lakini miaka 50 ijayo tumejipanga kuhakikisha tunatafuta masoko kabla bidhaa hazijazalishwa. Dunia ya leo haiuzi bidhaa zilizozalishwa, huzalisha bidhaa zinazohitajika na soko,” alisema Kapinga.

Ameongeza kuwa Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa kielelezo cha safari ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa kuonesha hatua iliyofikiwa na taifa pamoja na mwelekeo wa siku zijazo.