May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mpango aongoza mazishi ya Dada yake aliyemlea

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Phillip Isidori Mpango ameongoza mamia ya waombolezaji kumzika dada yake aliyemlea na kumsomesha shule ya msingi katika Kijiji cha Kipalapala, kata ya Itetemia mjini Tabora.

Ibada ya kumwombea marehemu Maria Isidori Mpango (82) imefanyika jana katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu, Parokia ya Kipalapala, Jimbo Kuu la Tabora na kufuatiwa na mazishi yaliyofanyika jirani na kanisa hilo.

Akitoa salamu kwa niaba ya wanafamilia Makamu wa Rais amesema marehemu alikuwa mtu muhimu sana kwake, alimlea katika maadili mema na kumwongoza vizuri katika maisha yake ikiwemo kumpeleka shule.

Amebainisha kuwa wamepokea msiba huo kwa mshtuko na majonzi makubwa kwa kuwa marehemu alikuwa zaidi ya dada, alikuwa mama na mlezi miongoni mwa wanafamilia.

Amewashukuru Watumishi wa Ofisi yake, taasisi mbalimbali, Viongozi wa chama na serikali, viongozi wa dini , wanaTabora , Kigoma, Buhigwe na kwingineko waliokuja kuwafariji katika msiba huo wa kuondokewa na ndugu yao.

Aidha amewashukuru Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Kitete, wauguzi na wafamasia kokote alikopita kupata huduma wakati wa ugonjwa wake  kwa juhudi zao kubwa za kuokoa maisha yake.

Akiongoza ibada ya kumwombea marehemu, kaka wa Makamu wa Rais, Padre Sebastina Isidori Mpango kutoka Jimbo la Florida nchini Marekani amesema licha ya dada yao kutwaliwa na Mungu kuna maisha baada ya kifo.

Amebainisha kuwa enzi za uhai wake marehemu alimpenda sana Mungu, ibada ilikuwa sehemu ya maisha yake, hakuacha kusali, alitambua kuwa siku moja ataondoka hapa duniani.

‘Dada alitamani uzima wa milele, ndio maana hakumwacha Mungu, amemaliza safari yake vizuri, sisi tuliobaki ni wajibu wetu kuendelea kujinyenyekeza mbele za Mungu ili siku ikifika tumalize mwendo salama’ amesema.  

Marehemu Maria Isidori alizaliwa mwaka 1941 na kufanikiwa kupata watoto 10 kati yao 8 wako hai, ameacha mgane, wajukuu zaidi ya 20 na vitukuu 5, Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.