Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MTANDAO wa Matawi ya Benki ya NMB nchini umezidi kutanuka, baada ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango kuzindua Tawi la 229 la NMB Buhigwe, alilosema linaenda kuchachua kasi ya ukuaji kiuchumi kwa wakazi wa Halmashauri hiyo, wakiwemo wadau wa Sekta za Kimkakati – hususani za Kilimo na Biashara.
Uzinduzi wa Tawi la NMB Buhigwe uliofanyika chini ya kaulimbiu ya: ‘Tunajivunia Kukufikia na Kukuhudumia,’ umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, ukienda sambamba na makabidhiano ya misaada ya vifaa vya elimu na afya vyenye thamani ya Sh. Milioni 82 kwa shule, hospitali na zahanati za Buhigwe, zikiwemo Shule za Sekondari Kahimba na Nyumbigwa, za Msingi Katema, Nyamiti na Zahanati ya Kasumo zote za mkoani Kigoma.
Mchango huo ukamsukuma Dk. Mpango kuitaja NMB kuwa ni Fahari ya Watanzania, sio tu kutokana na Gawio Rekodi la Sh. Bilioni 45.5 ililotoa kwa Serikali mwezi uliopita, bali ushiriki wa taasisi hiyo katika kutatua changamoto za jamii kupitia Program ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), ilikotenga takribani Sh. Bilioni 6.2 kusaidia Jamii kwa mwaka huu kutokana na faida yao ya mwaka uliopita wa 2022.
NMB Buhigwe linaifanya taasisi hiyo kinara ya fedha kufikisha matawi 132 wakati huu inapoadhimisha miaka 25 ya huduma na mafanikio ya kitaifa na kimataifa – hivi sasa ikiwa na wateja zaidi ya milioni 6, mbali na matawi 97 iliyokuwa nayo wakati ikianzishwa mwaka 1997, ikitambulika kama Benki ya Makabwela ilipokuwa na wateja 600,000 tu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, ulioshuhudiwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sadat Mussa, Dk. Mpango aliipongeza NMB kwa kuambatanisha tukio hilo na ukabidhi wa vifaa tiba na elimu, sambamba na kulitengea tawi hilo Sh. Bil. 1 ya kukopesha wateja na wadau wa mnyororo wa thamani wa Kilimo na Biashara, huku akiwataka Wana Buhigwe kuzichangamkia.
Dk. Mpango Ameongeza kuwa tawi hilo linaenda kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi, ikiwemo kumalizia changamoto ya mikopo migumu kutoka kwa wakopeshaji wadogo ‘kausha damu,’ upotevu wa pesa, uporaji na matumizi yasiyo ya lazima, lakini pia litavutia wawekezaji na kuwa chachu ya ongezeko la akaunti za wateja na kukuza pato la taasisi hiyo, hivyo kutanua Gawio la Serikali pamoja na fungu la Uwajibikaji kwa Jamii.
Licha ya kuishukuru na kuipongeza NMB, Dk. Mpango ameitaka benki hiyo kuendelea kuongoza taasisi zingine katika kufanikisha azma ya Serikali ya kusogeza huduma za kifedha kwa jamii kwa kukagua ili kubaini maeneo yanayostahili kufikishiwa matawi na mawakala, sambamba na kuwahimiza wakazi wa Buhigwe na Kigoma kwa ujumla kutumia huduma hizo zinapowafikia na kuachana na utunzaji fedha kwenye mitungi majumbani.
“Wito wangu NMB na wengine watakaofuata nyayo zenu kuja hapa, hakikisheni elimu ya fedha inawafikia wananchi, wengi wao hapa hawajui maana au faida za hisa na hati fungani. Hawajui umuhimu wa kukopa kwa malengo ndio maana wanaishia kutumia mikopo kwenda kunywea pombe au kuposea wake wa ziada.”BoT na Umoja wa Mabenki unaweza kuongeza nguvu eneo hilo la elimu ya fedha,” alisisitiza Dk. Mpango huku akiitaka NMB yenyewe kuchangamkia fedha za Mfuko wa Mazingira Ili kujiongezea nguvu ya kuimarisha mapambano ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kama inavyofanya kupitia Sh. Bilioni 2 ilizotenga kwa ajili ya Kampeni Endelevu ya Upandaji Miti Milioni moja kwa mwaka huu
Aidha, ameitaka NMB kwamba licha ya uimara na uthabiti wake kimtaji na kiuchumi, inapaswa kujiimarisha na kujiweka kinga zaidi za kudhibiti athari za misukosuko itokanayo na kuyumba kwa Sekta ya Fedha duniani kunatokana na mikwamo kama ya Majanga ya Covid na vita za kimataifa, ambako aliiagiza BoT kuweka mkazo wa kupambana na kuporomoka kwa Mabenki Ili kuyawezesha kuhimiri changamoto hizo kama ilivyo NMB.
Mapema kabla ya Dk. Mpango, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, amesema changamoto ya upotevu wa muda wa kufuata huduma za kifedha mbali imemalizwa, kama zitakavyomalizwa nyingine zilizokwaza ustawi wa kiuchumi wa wakazi wa Buhigwe, ambao wametengewa kupitia tawi lao hilo Sh. Bilioni 1 za mikopo ya kipindi kifupi inayoenda kuongeza thamani ya kilimo hasa kwa mazao ya kimkakati yanayolimwa hapo.
“Tawi limetengewa Sh. Bilioni 1 ya mikopo ya haraka kwa ajili ya kuongeza thamani kwenye mazao ya kimkakati yakiwemo mahindi, pamba, mpunga, kahawa, tangawizi, mihogo, chikichi na mengineyo, pamoja na Biashara na ujasiriamali. Hizi ni sehemu ya jitihada za Kimkakati za NMB kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alibainisha Mponzi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, amevutiwa na namna Wana Buhigwe walivyohudhuria kwa wingi, akiyaita mahudhurio hayo kama uthibitisho wa utayari na kiu ya huduma za kifedha miongoni mwao na kwamba benki yake iko tayari ikiwa na nguvu za kipesa kukidhi mahitaji ya Wana Kigoma aliowataka wajione kama wamililiki wa hisa za NMB kupitia asilimia 31.8 ya Hisa za Serikali, hivyo kuwasisitiza kuwa NMB ndio chaguo sahihi kwao.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Fedha wa BoT, Sadat Mussa, ameipongeza NMB kwa kusambaza elimu ya fedha na huduma za kibenki mjini na vijijini, na kwamba Sekta hiyo nchini inazidi kuimarika baada ya mkwamo wa Covid na Vita ya Ukraine, ambako jumla ya Sh. Trilioni 29 zimetolewa na taasisi za fedha kama mikopo hadi kufikia Juni mwaka huu, huku BoT yenyewe ikitenga Sh. Trilioni 1 kuyakopesha mabenki hayo.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â