May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mollel:Asanteni kwa kushirikiana nasi katika kuboresha sekta ya Afya

Na Mwandishi wetu, timesmajira

Naibu Waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel ameushukuru uongozi wa Shirika la afya la Japan, TOKUSHUKAI MEDICAL GROUP kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Mollel ametoa pongezi hizo leo Machi 14 alipokutana na uongozi wa Shirika hilo kutoka Japan katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.

“Ninawashukuru kwa namna mlivyoungana na Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo kikuu cha Dodoma, nchi ya Japani imekuwa ikisaidia katika kuboresha Sekta ya Afya kwa kuhakikisha huduma zinapatikana hasa katika matibabu ya figo. ” Alisema Naibu Waziri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa,Dkt. Alphonce Chandika ameeleza jinsi TOKUSHUKAI MEDICAL GROUP ilivyo isaidia Hospitali ya Benjamin Mkapa.

“Hospitali ya Benjamin Mkapa imejengewa uwezo wa kufanya huduma ya upandikizaji figo na Shirika hili mpaka sasa tunajivunia kwa kupandikiza wenyewe hii ni kwasababu ya TOKUSHUKAI MEDICAL GROUP ” amesema Dkt Chandika

Aidha Mwenyekiti wa wa TOKUSHUKAI MEDICAL GROUP Prof. Higashiue Shinichi ameeleza jinsi walivyo pokelewa na taasisi hizi mbili UDOM na BMH na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha Sekta ya Afya.

“Nasi tunashukuru kwa tulivyo pokelewa, kama tusingekubaliwa kutoa huduma hii leo tusinge kuwa hapa tukifurahia kuadhimisha miaka mitano ya upandikizaji figo” amesema Prof. Shinichi.