April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Gwajima akutana na Menejimenti ya Wizara yake,wapanga mikakati

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesema pamoja na mambo mengine Wizara yake ina jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu kwa kuelimisha jamii ili ichane na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinachangia watoto kuondoka majumbani kwao na kukimbilia mitaani na hivyo kuzalisha watu ambao hawana Tija kwa Taifa.

Dkt.Gwajima ameyasema hayo jijini hapa alipokutana kwa mara ya kwanza na Menejimenti ya Wizara yake tangu iRais Samia Suluhu Hassan alipoitenganisha kutoka iliyokuwa Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto .

“Ili jamii iendelee pia inatakiwa amani na utulivu ,hivyo ni vitu mtambuka ambavyo  pia wizara ya maendeleo ya jamii inaingia…, kwamba tunawekaje mifumo inayoifanya jamii yetu isiwe na ukatili,

“Katika eneo la mtoto kuna haki tano za mtoto ikiwemo  kulindwa tangu akiwa tumboni ,kuzaliwa mpaka kukua inatazamwaje na ina sheria yake,

“Mtoto huyu asipoandaliwa vizuri kwenye familia,malezi ya familia yakoje ,hivi juzi tulizindua mkakati wa malezi na makuzi ya mtoto ambaye anaweza akakatiliwa kwa sababu familia haijaandaliwa ,atakimbia nyumbani atakwenda mtaani halafu tutapata wimbi kubwa la watoto wa mtaani,maendeleo ya jamii hayatokea kwa sababu hawa sasa watakuwa wanaishi kwenye mazingira hatarishi na wala hawachangii vizuri kwenye Taifa lao”amesema na kuongeza kuwa 

“Vitendo hivi vya ukatili vinafanya kunakuwa hakuna utulivu wa kuweza kuyafanya maendeleo yaende mbele kwa sababu kuna watu fulani hawajaandaliwa vizuri na hivyo kusababisha hasara kwa Taifa.”

Amesema, ili kuleta amani na utulivu Wizara yake inaingia hapo kwani ina mifumo yake kuanzia ngazi za chini ya kamati za ulinzi ,mabaraza ya ulinzi wa watoto na wanawake huku akitaka mabaraza hayo yaamshwe na yawezeshwe ili yafanye kazi zake ikiwemo kuelimisha jamii ili  iweze kuwa na amani na kujiamini lakini pia kuishi bila hofu na badala yake kutulia na kufikiria  maendeleo kwenda mbele .

Vile vile amesema  pia kuna masuala mengine yanayotakiwa kufanyiwa kazi ni pamoja na suala la maafisa maendeleo ya Jamii warudi kufanya kazi yao waliyoisomea .

“Changamoto hizi zipo tunatakiwa tuzifanyie kazi ,na Mheshimiwa Rais ameelekeza hadi ya watu hao irudi juu,waonekane na wafanye kazi zao walizosomea ,ni jukumu la katibu Mkuu kutazama na kutafuta kila fursa kuona kwamba wanaajiriwaje maana hawatoshi na nchi hii ni kubwa.”

Dkt.Gwajima amesema ,lengo kuwapata Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kutosha na waonekane na kuelimisha jamii ili iweze kubadili fikra na kuja na mifumo yake yenyewe.

Pia amesema zipo sera nyingi ambazo zimepitwa  na wakatihuku akiztaja baadhi yake kuwa ni pamoja na sera ya maendeleo ya jamii,masuala ya wanawake ,makundi maalum,wazee na watoto.

“Zote hizi zimepitwa na wakati ,sasa hii ni fursa tutawaunganisha wananchi wote na wadau ili kuja kuziangalia ili haraka zaidi tupate sera na miongozo inayoendana na wakati tuliopo sasa .”amesisitiza Dkt.Gwajima