December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Gwajima aeleza namna serikali inavyopambana kuwanusuru watoto waishio katika mazingira magumu

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesema pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali pamoja na wadau wengine ya kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama,lakini bado kuna watoto wengi wanaoishi kwenye mazingira hatarishi (mitaani) .

Dkt.Gwajima ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Makao ya Watoto Home of Love and Joy (Upendo) yaliyopo Hombolo jijini Dodoma.

Hata hivyo amesema,Serikali kwa kushirikiana na wadau wake inaendelea kutafuta ufumbuzi kwa kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali wanaofanyia kazi eneo hilo.

Aidha amesema,Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan  inaangalia kwa jicho la karibu sana na uzito mkubwa suala la maendeleo ya watoto ambapo imezindua program mpya kubwa tatu kwa ajili ya mandeleo na ustawi wa watoto.

Dkt.Gwajima alitaja Programu hizo kuwa ni pamoja na Programu  ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambayo ni ya kwanza Afrika Mashariki yenye lengo la kuhakikisha watoto wanapata malezi na kukua katika maadili, uzalendo pamoja na kuipenda na kuitumikia nchi yao.

Aliutaja mkakati mwingine kuwa ni Mkakati wa malezi kwa watoto ambao ulizinduliwa sambamba na uzinduzi wa  Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo ambayo ni ya kipekee Afrika Mashariki na Kati.

Kwa mujibu wa Gwajima pia katika kuhakikisha kuwa kipindi cha utoto kikiisha mtoto hapotezi dira ya maendeleo,ilizinduliwa  Agenda ya Kitaifa ya kuwekeza kwenye Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe huku akisema mikakati yote hiyo imezinduliwa mwaka 2021.

Akizungumzia sababu za watoto kukimbilia mitaani Dkt.gwajima alisema moja ya sababu hizo ni pamoja na ukatili wa majumbani ambapo matokeo yake wanakutana na aina nyingine za ukatili na mazingira hatarishi zaidi.

“ Takwimu zinaonesha waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili kwa upande wa watoto 70% ni wa kike….,tukumbuke kuwa, watoto wanapokuwa wanaishi kwenye mazingira hatarishi pamoja na changamoto nyingi pia wanakutana na ukatili mkubwa. “amesema Dkt.Gwajima

Amesema,pamoja na serikali na wadau wake kuendelea kupambana kuzuia ukatili pia inatoa huduma kwa wahanga wa ukatili ikiwemo huduma ya kisheria ambapo kwa mwaka 2020/21 mashauri 3889 yamepelekwa Mahakamani na 1,504 yametolewa hukumu na mengine kazi inaendelea.

 Aidha, ukiacha ukatili kwa watoto hata watu wazima wanafanyiwa ukatili ambapo wanawake wanatengeneza 96% ya wanaoathirika huku akisema, kwa ujumla wakeukatili kwa mtu yeyote haukubaliki.

“Hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wake wote itaendelea kuimarisha utekelezaji wa afua zenye kuhamasisha kuzuia na kushughulikia aina zote za ukatili,”alisema na kuongeza kuwa

“Lengo ni kuhakikisha jamii ya kitanzania inafurahia haki ya kuishi ambapo baadhi ya hatua zinazoendelea kutekelezwa ni pamoja na kuendelea kujenga uelewa kwa jamii ya kitanzania kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia ili jamii yenyewe iweze kuchukua hatua za kukataa na kuepuka mambo ya ukatili na pia jamii iweze kutoa taarifa pale wanapoona viashiria au vitendo vya ukatili.”

Vile vile amesema, ni jukumu la Serikali kuimarisha uratibu wa wadau wanaotekeleza afua za kuzuia na kushughulikia ukatili sambamba na kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za viashiria au matukio ya ukatili katika familia na jamii lakini pia ‘kuendeleza Kampeni ya TWENDE PAMOJA UKATILI SASA BASI’ ili kila mdau kwa nafasi yake aweze kuelimisha jamii juu ya athari za vitendo vya ukatili na jinsi ya kuzuia ukatili.

Naye Naibu Katibu Mkuu Amon Mpanju alitumia fursa hiyo kuiasa jamii kuwa na moyo wa kujitolea katika vituo vya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za wadau wanaofanya kazi katika eneo hilo.

Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Sista Mkuu wa Makao ya Watoto Upendo ,Sista  Radience alisema,kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha za uendeshaji wa kituo hicho pamoja na gharama za umeme.

Pamoja na kuushukuru ugeni huo,Sista Radience aliiomba Serikali kukisaidia kituo hicho solar ili kupata uhakika wau meme na kupunguza gharama za uendeshaji wa kituo.

Vile vile ameiomba Serikali kuwapatia Bima ya Afya walengwa wa kituo hicho ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu.

Ziara hiyo ya Dkt.Gwajima na Menejimenti ya Wizara yake,ni mwendelezo wa ziara ambazo ameanza Januari 17 mwaka huu ya kutembelea makao ya watoto kwa lengo la kujifunza lakini pia  kutambua changamoto katika makao ya watoto na kuzipatia ufumbuzi.