Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amemwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo jipya Katoliki la Mafinga, Mhashamu Vincent Cosmas Mwagala.
Dkt. Beteko ameeleza kuwa, Dkt. Samia anaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhahebu mengine ili kuwaletea maendeleo Watanzania.
Amesema, nia ya Rais, Dkt. Samia ni kuona wananchi wanapata huduma bora katika nyanja mbalimbali ikiwemo Zahanati, Barabara, Maji, Shule na Umeme wa uhakika hivyo ili kutekeleza suala hilo kwa ufanisi Serikali inashirikiana na Taasisi binafsi ikiwemo madhehebu mbalimbali ya dini katika kuwapelekea maendeleo wananchi. n.k
Akizungumza na Wananchi waliohudhuria sherehe hiyo katika Halmashauri ya Mafinga, Wilayani Mufindi mkoani Iringa, Dkt. Biteko amesisitiza kuhusu utunzaji wa mazingira na kutoa angalizo kuwa yeyote anayeharibu mazingira lazima aonekane kama adui na achukuliwe hatua kwani athari za kutokutunza mazingira ni kubwa, akitolea mfano kuwepo kwa mgawo wa umeme kutokana na kutokuwa na maji ya kutosha kuzalisha umeme.
“Leo tumejenga mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere, mradi ule ni mkubwa sana, lile si bwawa tu bali ni ziwa kwani urefu wake ni kilometa 100 na upana wake ni kilometa 25.
“Uwepo wake unahitaji maji na ikizingatiwa kuwa gharama nyingi zimetumika kujenga mradi huo zaidi ya shilingi Trilioni Sita, ni lazima tulinde mazingira ili kupata faida mbalimbali ikiwemo maji ya kutosha kuzalisha umeme.” Amesema Dkt. Biteko
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa tarehe 19 Machi, 2024, Rais, Dkt. Samia ametimiza miaka mitatu akiwa madarakani ambapo amedhihirisha kwa vitendo kuwa ni kiongozi bora ambaye ameendelea kuiweka nchi katika hali ya utulivu.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia ameendelea kutekeleza miradi mbalimbali aliyoikuta mara baada ya kuapishwa ikiwemo barabara, reli, umeme na ameendelea kubuni miradi mipya na kuiendeleza kwa kasi kubwa.
Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Dini na Watanzani kumuombe Rais Samia ili aendelee kuongoza nchi kwa ufanisi akiwa na afya njema na pia kuiombea nchi ili iendelee kuwa ni mahali salama pa kuishi.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuchagua viongozi wanaokerwa na shida za wananchi na wanaozitatua na kwamba wasichague viongozi kwa kigezo cha ukabila, dini au mahali walipotoka bali msingi uwe ni maendeleo na utanzania.
Kwa upande wake, Askofu Mpya wa Jimbo la Mafinga, Mhashamu Vincent Mwagala amesema Kanisa Katoliki litaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika masuala ya ya ustawi wa jamii ili amani iendelee kutamalaki na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuhudhuria sherehe hiyo na kuwasilisha ujumbe wenye matashi mema kutoka kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile na Spika Mstaafu, Mama Anna Makinda.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi