May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA yajivunia miaka mitatu uongozi wa Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), inajivunia mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha miaka mitatu tokea aingie madarakani.

Kwa ufupi, mafanikio hayo ni pamoja na kuunganisha umeme kwa vijiji 5,481 na kufanya vijiji vyenye umeme kufikia 11,843 sawa na
asilimia 96.14 ya vijiji vyote nchini ambavyo ni 12, 318.

Vilevile, vitongoji 5,562 vimefikishiwa huduma ya umeme na kufanya vitongoji vyenye umeme kufikia 32,750 sawa na asilimia 51 ya vitongoji vyote nchini ambavyo ni 64,760.

Aidha, vitongoji vingine 8,150 vitafikishiwa umeme kupitia Miradi ya Ujazilizi kabla ya kuisha mwaka 2025.

Kwa upande wa nishati safi ya kupikia, hadi sasa REA imewezesha ugawaji wa Mitungi ya Gesi (LPG) na vichomeo vyake 83,500.

Vilevile, ndani ya Mwaka wa Fedha 2023/24, REA
itagawa kwa bei ya ruzuku, Mitungi ya Gesi takribani 450,000 pamoja na kujenga mifumo ya nishati safi ya kupikia kwa Taasisi
100 zinazohudumia watu zaidi ya 300.

Miradi hii ni endelevu na itatekelezwa kila mwaka ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hasan katika azma yake ya kumtua mama mzigo wa kuni, kulinda misitu, kuzuia mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kulinda afya za Watanzania.