Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online-Bukoba
Katika jitihada za kujenga maadili mema ndani ya jamii, Watanzania wametakiwa kujipambanua kupitia dini zao na kuzitumia kama nyenzo muhimu ya kuimarisha misingi ya maadili ambayo kwa sasa yanaonekana kumomonyoka.
Rai hiyo imetolewa Mkuu wa Kanisa la Kiinjiki la kilutheri Tanzania ( KKKT ),Askofu Dkt. Alex Malasusa,katika mahafali ya kidato cha sita ya mwaka 2026 ya shule za sekondari Kaizirege na Kemebos, zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Dkt.Malasusa amesema kuwa kupitia ushirikiano wa viongozi wa dini zote, taifa lina nafasi kubwa ya kujengwa katika misingi imara ya maadili, akisisitiza kuwa umoja uliopo licha ya tofauti za dini na makabila ni tunu adhimu ya Tanzania.
Amesema Tanzania inahitaji umoja sio kuonyoosheana vidole na kebehi kwa sababu ya dini.Dini ni urithi ambao wengi wameupokea, hivyo hakuna sababu ya kugeuzana kuwa maadui kwa misingi hiyo hivyo ni wakati wa watu kupewa elimu ya kumjua Mungu.
“Watu wamjue Mungu kama vile ilivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,viongozi wanapochaguliwa na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali wanaapa kwa kutumia dini zao,hivyo tuwaone wakitenda mambo sawa na viapo vyao, mtu asiape kwa Biblia na Quran halafu hafanyi kile alichokiapa,”amesema Dkt.Malasusa na kuongeza:
“Tuwakatae wanaovunja amani kwa makusudi, tusiwaonee aibu,viongozi wa dini lazima tuwaonye watu wa namna hiyo na tuzungumze nao ili tuwasaidie.Tuwatie moyo wote wanaotafuta amani kwa juhudi kwani ni kitu muhimu kwa taifa,”.
Sanjari na hayo amempongeza muwekezaji wa shule za Kaizirege na Kemebos kwa kuwekeza katika sekta ya elimu,ambapo ameeleza kuwa si jambo la kawaida kwa watu wengi kufanya uwekezaji wa aina hiyo. Ameeleza kuwa shule hizo zina mchango mkubwa katika kuandaa vijana watakaolitumikia taifa.
Vilevile aliwapongeza akina mama kwa juhudi zao za kusimamia elimu ya watoto wao, akieleza kuwa wao wamekuwa mstari wa mbele katika kusindikiza safari ya elimu, huku akitoa wito kwa wazazi, hasa baba, kushiriki kikamilifu zaidi katika malezi na elimu ya watoto wao.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule za Kaizirege na Kemebos, Kisha Ilamulila, amesema taasisi hizo zilianzishwa mwaka 2007 na muwekezaji mzawa Eusto Ntagalinda, na kwa sasa zinatoa elimu kuanzia ngazi ya chekechea hadi kidato cha sita.Shule hizo zina walimu wenye sifa, miundombinu ya kisasa na mazingira bora ya kujifunzia.
Ilamulila amesema kuwa jumla ya wanafunzi 212 wanahitimu kidato cha sita mwaka 2026, wakiwemo wasichana 86 na wavulana 126. Ameeleza kuwa wanafunzi hao wamejiandaa vizuri kwa mitihani yao ya kitaifa inayotarajiwa kuanza Mei 4 mwaka huu, baada ya kufanya mitihani mbalimbali ya majaribio ya ndani na nje ya shule.
Ameongeza kuwa shule zina maabara za kisasa kwa ajili ya masomo ya sayansi kwa vitendo, pamoja na zahanati iliyosajiliwa Februari 8, 2025 na Wizara ya Afya, inayotoa huduma za kwanza kwa walimu, wanafunzi na wafanyakazi.

Kwa upande wa wahitimu, kupitia risala yao iliyosomwa na Elizabeth Mmassy, wamesema wamejiandaa kikamilifu kufanya mitihani yao ya mwisho na kuahidi kufanya vizuri. Wameeleza kuwa siri ya mafanikio yao ni bidii katika masomo, nidhamu na kumtanguliza Mungu katika kila wanachofanya.


More Stories
DCEA yateketeza ekari 68 za bangi Tabora
Mapinduzi saratani Mbeya kwa takwimu sahihi
Wajumbe wa Bodi ya REA waipongeza ETDCO