May 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UNESCO, MAIPAC watoa mwongozo kwa wanahabari

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Arusha

KATIKA hatua inayolenga kulinda utu na heshima ya jamii za pembezoni, Shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi na utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari wa kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC) pamoja na Idara ya Habari–Maelezo, wameanza maandalizi ya mwongozo maalum kwa wanahabari na watengeneza maudhui, utakaoelekeza namna sahihi ya kuripoti.

Mwongozo huo unatarajiwa kuwasaidia wanahabari na watengeneza maudhui kutambua maadili, mila na miiko ya jamii za Wahadzabe, Wamasai, Wadatoga na Wakie kabla ya kuandaa na kusambaza taarifa zinazowahusu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma amesema hayo wakati akizungumza katika mjadala wa maadhimisho ya World Press Freedom Day jijini Arusha, uliojadili nafasi ya watengeneza maudhui mitandaoni na matumizi ya akili unde.

Amesema katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko la watengeneza maudhui wa ndani na nje ya nchi wanaoingia moja kwa moja katika maeneo ya jamii hizo na kurekodi au kusambaza maudhui bila ridhaa yao, hali inayokiuka maadili na wakati mwingine kudhalilisha utu wao.

“Kutokana na changamoto hii, MAIPAC kwa kushirikiana na UNESCO na Idara ya Habari–Maelezo wanaandaa mwongozo maalum wa kufanya kazi katika jamii hizi kwa kuzingatia maadili na kulinda utu wa wananchi hao,” amesema Juma.

Amesema sambamba na hatua hiyo, taasisi hizo kwa kushirikiana na SAVVY Media zinatarajia pia kujenga uwezo kwa jamii hizo katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili ziweze kunufaika kiuchumi na maudhui yanayowahusu.

“Tutazijengea uwezo jamii hizi kutumia mitandao kwa manufaa yao, kutambua haki zao za kidigitali na hatimaye kuboresha maisha yao kiuchumi,” amesema.

Wakichangia mjadala huo, baadhi ya watengeneza maudhui pamoja na maafisa kutoka Tanzania Communications Regulatory Authority wamesema matumizi ya mitandao ya kijamii na akili unde yanapaswa kuwa nyenzo ya maendeleo kwa vijana na jamii, badala ya kuibua hofu au madhara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe katika bonde la Eyasi, wilayani Karatu, Mdindi Samboga amesema jamii hiyo imekuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii lakini haijanufaika ipasavyo.

Amesema mara nyingi watu hufika katika maeneo yao, kuchukua picha na kufanya mahojiano, lakini faida ya maudhui hayo hubaki kwa waliotengeneza bila kuwanufaisha wahusika.

“Tunawaona wanakuja kutupiga picha na kutuhoji, tunaambiwa mijini tunaonekana sana, lakini sisi hatunufaiki zaidi ya kupewa vitu vidogo kama pombe, tunaomba sasa tusaidiwe kunufaika,” amesema Samboga.

Hatua hiyo ya kuandaliwa kwa mwongozo inatarajiwa kuwa mwanzo wa mabadiliko katika namna vyombo vya habari na watengeneza maudhui wanavyoshughulikia taarifa za jamii za pembezoni, huku ikilenga kulinda haki, hadhi na ustawi wa jamii hizo.