Na Mary Margwe,TimesMajira Online Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Dkt.Suleiman Serera amewaonya baadhi ya madiwani na wenyeviti wa vijiji kuacha mara moja tabia ya kujihusisha na uuzaji wa ardhi unaosababisha kuwepo kwa migogoro na kurudisha nyuma maendeleo.
Hayo ameyasema alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi chini ya Mwenyekiti wake, Baraka Kanunga, DC huyo alisema yeyote atakayekaidi hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Dkt.Serera amesema, japo yeye ni mgeni, lakini hana ugeni katika kazi, hivyo alitoa onyo kwa mara ya kwanza na ya mwisho kuacha kabisa kujihusisha na tabia ya uuzaji wa ardhi, ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na imani na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Naomba tuelewane siku zote uhuru wako unapoishia ndio haki ya mwingine inapoanzia, uhanaharakati wa kiuongozi unapokua mwingi ndio mambo ya kutiana ndani yanakuja kila mmoja anazungumza hivi, hivi hamjui kama mimi ni DC, sasa haya yanatoka wapi, ili kila mmoja asiweze kufika huko lazima kila mmoja ajitambue mipaka yake inaanzia wapi na inaishia wapi, tukienda hivyo kwa kutambuana mipaka yetu naona mambo yatakua mazuri,” amesema Dkt. Serera
Tuhangaikie kutatua changamoto, lakini sio kwenda kubariki kufanya makosa juu ya makosa, watu wanakamatwa Mheshimiwa Diwani wewe ndio unakimbia wewe polisi kwa OCD kwenda kuwaombea wale waliofanya makosa, unatumia cheo chako vibaya, ugomvi sio wa kwako kwa nini wewe unaangaika damu zikurukie.
“Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya nilishakutana naye na kumweleza haya juu ya baadhi ya madiwani hao wenye uchu wa kuuza ardhi na kuzua migogoro,”amesema Serera.
Amesema, tabia ya kamatakamata na kuwaweka ndani madiwani siyo nzuri, hivyo kabla hawajafika huko kwenye hatua hiyo ni vyema wakaachana na tabia hiyo.
“Tunapaswa kusimama kwenye maendeleo na siyo kuzua migogoro isiyo na tija kwa kuuza ardhi za wananchi na kusababisha vurugu kwa jamii inayotuzunguka,”amesema Dkt.Serera.
Amesema, tangu awasili kwenye wilaya hiyo ameshakutana na madiwani 11 kati ya 18 wa kata zinazounda wilaya hiyo na ameona baadhi yao wenye kiu ya maendeleo wanavyosimamia maendeleo.
“Nimefika baadhi ya kata ikiwemo Mirerani kwa Salome Mnyawi amefanya kazi nzuri kwenye madarasa, Lucas Zacharia Kata ya Endiamtu na wengine wanafanya kazi nzuri,” amesema Dkt.Serera.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga alisema, madiwani wa halmashauri hiyo wanampokea kwa mikono miwili na watampa ushirikiano.
Kanunga alisema, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo hivyo watashirikiana na mkuu huyo wa wilaya ili kufanikisha maendeleo hayo.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu