May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Ilala atoa agizo kwa walimu wakuu

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

MKUU wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija amewataka Walimu wakuu wa Elimu Sekondari Wilaya ya Ilala wanapokamilisha ujenzi wa madarasa wawe wamekamilisha madawati yote ya Wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya Ludigija alitoa agizo hilo katika ziara yake ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya iliyoshirikisha Chama cha Mapinduzi kuangalia Utekelezaji wa Ilani ya chama katika fedha iliyotolewa na Serikali bilioni 5.1 kujenga madarasa 255 na madawati kila shule.

“Naagiza Wakuu wa shule ambao wanajenga madarasa ya UVIKO wakamilishe madarasa pamoja na madawati ,Mkuu wa Shule ambaye atashindwa kutekekeza agizo hili katika Wilaya yangu nitamtumbua atakuwa amejifukuzisha kazi Mwenyewe” alisema Ludigija.

Amewataka wakuu wa shule wote kushirikiana kwa pamoja fedha zipo kunapotokea changamoto watoe taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza katika sekta ya Elimu fedha hizo watasimamia na kualikisha ujenzi wote unakwisha kwa wakati.

Alisema katika Wilaya ya Ilala ina kata 36 katika kata 36 wamefanikiwa kujenga madarasa 255 katika shule 36 za sekondari.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala Ubaya Chuma alipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam,Watendaji na Viongozi wa Wilaya ya Ilala kwa utekelezaji wa Ilani ya chama.

“Nawapongeza Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam Mkurugenzi na watendaji wako kwa usimamizi mzuri madarasa yote yamemalizika kwa wakati ndani ya Halmashauri yetu ya Jiji sasa tujiandae kupokea Wanafunzi waweze kusoma ” alisema chuma.

Meya Halmashauri ya Jiji Omary Kumbilamoto alisema Halmashauri yake imeelekeza fedha shilingi bilioni 5.1 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya madarasa na kila Kata shule zimejengwa.

Mkuu wa Wilaya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija akisalimiana na Diwani wa Viti Maalum Wanawake Wilaya Ilala Asha Johari katika ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kutembelea Jimbo la ILALA kuangalia ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari
Mkuu wa Wilaya Ilala Ng’wilabuzu Ludidija (kulia)akiongea na Mbunge wa Jimbo la ILALA Mussa Zungu Shule ya sekondari Benjamin Mkapa kuangalia ujenzi wa madarasa ya sekondari
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Omary Kumbilamoto. (Kushoto)akiongea na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika ziara ya Kukagua ujenzi wa madarasa ya shule ya sekondari ,ziara hiyo imeandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija ambayo imewashirikisha Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala kuangalia utekelezaji wa Ilani (Katikati )Mwenezi wa CCM Ilala Said Sidde(PICHA NA HERI SHAABAN)