January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC asisitiza matumizi mazuri ya fedha za miradi

Na Hadija Bagasha Tanga,timesmajira,online

MKUU wa wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa amewataka madiwani wa Halmshauri ya jiji la Tanga kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha zinazotolewa kwajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi. 


Mgandilwa ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani cha kupitia taarifa za hesabu za mwisho kwa mwaka wa fedha 2020/21.


Mgandilwa amesema fedha nyingi za miradi ya maendeleo zinaweza kutumiwa vibaya ikiwa madiwani watashindwa kutekeleza wajibu wao wa kuangalia thamani ya kiwango cha fedha kinachotumika.

 
Aidha DC Mgandilwa amesema ni wajibu wa madiwani kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya fedha zinazotolewa kwenye miradi inayotekelezwa kwa kuhakikisha wanasimamia kiwango cha fedha kilichotolewa na kazi husika iliyofanyika. 

Katika kikao hicho Naibu Meya wa jiji hilo Joseph Colvas amesema kuwa watahakikisha madiwani wote wanasimamia ipasavyo fedha zinazotolewa kwenye miradi lengo likiwa kuharakisha maendeleo ya wananchi kwa haraka lakini pia kusimamia vyema fedha za umma. 


“Ni jukumu letu sisi madiwani tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa na madiwani wengine katika maeneo mengine juu ya matumizi yetu katika makusanyo na hata matumizi ya fedha za miradi niwaase madiwani wenzangu tuchape kazi tuzitumie kwa malengo yaliyokusudiwa fedha zinazotolewa kwajili ya wananchi wetu, “alisisitiza Naibu Meya Colvas.

 
Katika kikao hicho Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja Mstaafu Hamisi Mkoba amewataka madiwani wa jiji la Tanga kujitafakari na kuhakikisha katika vikao vyao wanajadili vitu vyenye tija kwa wanachi wao.”Mkoa wa Tanga umepata viongozi wapya,tumepata mkuu wa mkoa mpya,tumepata mkuu wa wilaya mpya na tumepata mkurugenzi wa jiji mpya nataka wasome haya mambo na wasome hawa watu wanataka nini katika kuliendesha baraza la madiwani,pamoja na kuendesha jiji la Tanga,


Aidha Mwenyekiti Mkoba amewataka madiwani hao kuhakikisha wanapitia kwa kina taarifa hiyo ya fedha waliyofikishiwa ili kuweza kuhoji pale watakapoona panahitaji kufanyiwa marekebisho. “Nieaambie tu kuwa Mh.Rais amekuwa anapigia makelele na kusisitiza maamuzi katika vikao sasa kama tunakuja tunakaa dakika tano..dakika mbili tunasema tumemaliza inakua hakuna litakalofanyika”alisema Meja Mstaafu Mkoba