March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Corona imechangia uhaba wa mafuta’

Na Zena Mohamed, Timesmajira Online,Dodoma

WAZIRI wa Kilimo, Prof.Adolf Mkenda,amesema pamoja na sababu zingine lakini Ugonjwa wa Corona umechangia kuyumba kwa soko la mafuta duniani kote kutokana na kusuasua kwa uvunaji na kuwa mzigo kwa walaji.

Mkenda amesema hayo jijini hapa wakati akifunga Wiki ya Taasisi ya PASS Trust (Private,Agriculture Sector Support Trust) iliyoandaliwa na taasisi hiyo kuanzia Julai 21 hadi Julai 24 kwa lengo la kuchagiza masuala ya kilimo nchini.

Wiki hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuwakutanisha wakulima,wauza zana za kilimo,taasisi za kifedha,wauza pembejeo,viongozi wa Serikali na wachakataji katika kuzungumzia masuala ya upatikanaji wa fedha kama kichocheo cha ukuaji wa kilimo biashara.

Amesema, ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia nchini,Serikali inatarajia kuleta mbegu bora za alizeti na kuzigawa kwa mkataba kwenye viwanda vinavyozalisha zao hilo hali itakafanya soko hilo kuwa la uhakika na kuondoa uhaba wa mafuta unaojirudia kila mwaka.

“Baada ya Viwanda kupewa mbegu hizo vitapaswa kuingia mkataba wa makubaliano na wakulima wakubwa au vyama vya ushirika kisha kuwakabidhi mbegu hizo bila malipo ili kutoa fursa ya kuongea malighafi.

“Na sisi kama Serikali tutawajibika kuwawezesha wakulima kwa kuwapelekea wataalamu wa zao la alizeti,na tutaweka masharti kwamba ukivuna alizeti unamuuzia mwenye kiwanda ili kuhakikisha viwanda vyote vinavyoingia mkataba vinazalisha mafuta kwa mwaka mzima,”amesema.

Ameeleza kuwa kwenye kilimo hatua hiyo ni fursa kwa kuwa Tanzania itakuwa na uwezo wa kuzalisha mafuta na kuuza nje ya nchi.

“Uzalishaji mdogo wa alizeti unachangia usambazaji kupungua wakati mahitaji yapo palepale huku bei ikipanda na kuwanyonya wananchi, lazima viwanda vyetu viwe na malighafi kuwezesha kufanya kazi kwa Mwaka mzima na Kutoa ajira kwa Vijana,”amesema Mkenda.

Pia alizitaka benki zote nchini kutoa fursa ya mikopo kwa wakulima na kushusha riba ili kuchochea kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wakulima wengi zaidi kukifanya Kilimo kuwa biashara.

“Ukitaka kupambana na umaskini Tanzaniana, unaweza kufanya mambo mengi Sana lakini ukweli ni kwamba umaskini utaaisha kwa kilimo,ukitaka mali utaipata shambani,”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo, Tausi Akida amesema kuwa changamoto za mitaji kwa wakulima nchini bado zipo nyingi na kwamba ipo haja kwa Taasisi za fedha kuongeza kiwango kwa wakulima.

Amesema katika mikopo hiyo trilioni 19 inayotolewa kwa mwaka, ni mikopo trilion 1 ndio huelekezwa kwenye mahitaji ya kilimo.

“Suala hili bado ni muhimu ili kuweka tija kwenye mazao ya kimkakati tunapaswa kongeza nguvu Katika kukuza zao la alizeti na zabibu ili kusapoti viwanda vya uchakataji ,kwa upende wetu tumeanza na programu kwa mikoa ya Simiyu,Dodoma,Singida na Morogiro kwa Kutoa pembejeo,”ameeleza

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema mkoa huo unatarajia kusajili Kaya laki 3 zinazostahili kufanya kilimo biashara na ili Kufanikisha maendeleo ya kilimo na kuwa fahari jiji hapo.

Ametaja mazao ya zabibu na alizeti kuwa ya kimkakati na kwamba ili Kufanikisha hilo atatumia nafasi yake kushauriana na Wizara ya kilimo kuona namna ya kuongeza ufanisi kwa mazao hayo

Hata hivyo Mtaka amewataka wananchi kuendelea kujilinda na wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona huku akitumia kauli ya “Uhai wako sio Mali ya Serikali ,ukifa Serikali inabaki,usisubiri kusukumwa jiepushe na misongamano isiyo lazima ,fuata taratibu zote za kiafya,pi maeneo yote ya kutolea huduma za kijamii kuwe na maji tiririka,”pamoja na kutumia fursa hiyo kugawa barakoa kama ishara ya kueneza ujumbe kwa jamii kujikinga zaidi.