January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yataka miradi halmashauri ikamilishwe kwa mapato ya ndani

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC) kutoka Mkoa wa Tanga Mohamed Salim maarufu Ratco amezitaka halmashauri zisisubiri fedha kutoka Serikali Kuu bali zitumie mapato ya ndani kukamilisha miradi kwani nchi ni kubwa na mahitaji ya huduma za jamii ni makubwa.

Kauli hiyo ameitoa baada ya kutembelea Kituo cha Afya Mgombezi kilichopo Halmashauri ya Mji Korogwe na kukuta baadhi ya huduma kama vile mifumo ya maji ndani ya kituo hicho haijakamilika ikiwa ni ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Tanga ya kutembelea halmashauri zote 11 za mkoa huo ili kukagua miradi inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo pia walitembelea zahanati ya Lwengera- Darajani.

MNEC kutoka Mkoa wa Tanga Mohamed Salim (wa tatu kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mgombezi Halmashauri ya Mji Korogwe Dkt. Paulo Anyabwile (kushoto).

Hivyo ameitaka halmashauri kuweka mfumo wa mabomba kwa fedha za mapato ya ndani badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu.

“Mkurugenzi baadhi ya huduma mnatakiwa muweke kwa fedha zenu za mapato ya ndani nchi hii ni kubwa na miradi kwa ajili ya huduma za jamii ipo nchi nzima,”amesema Salim.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Tito Mganwa amekubaliana na MNEC kuwa baadhi ya huduma ikiwemo kuweka mfumo wa maji ya bomba watatumia kwa fedha za mapato ya ndani.

Huku amesisitiza kuwa kama watatumia fedha za mapato ya ndani kwa shughuli zote zilizobaki hapo halmashauri itashindwa kujiendesha.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Kituo cha Afya Mgombezi, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Paulo Anyabwile amesema halmashauri hiyo Juni 8, 2021, ilipokea kiasi cha milioni 250 kwa ajili ya ujenzi na utekelezaji ulianza mwaka wa fedha 2021/2022 kwa Force Akaunti.

“Mradi huu ulikadiriwa kutumia zaidi ya milioni 262 kwa majengo mawili,zaidi ya milioni 122 kwa jengo la upasuaji na zaidi ya milioni 140 kwa jengo la wazazi,ulianza rasmi kutekelezwa Oktoba 13, 2021 na kukamilika Januari 12, 2022 kwa asilimia 98 hivyo kugharimu milioni 249 ambapo fedha hizo hazikukamilisha mradi,”.

Hivyo amesema zaidi ya milioni 36 zinahitajika ili kukamilisha mradi kwa ajili ya ujenzi wa mashimo mawili ya vyoo, kuingiza umeme awamu ya tatu, uwekaji wa sluice na scrub sink na uwekaji wa sakafu ya epoxy.

Dkt. Anyabwile amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023, halmashauri ilipokea kiasi cha milioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambapo tayari vimekwisha nunuliwa na kituo kinatoa huduma.

MNEC kutoka Mkoa wa Tanga Mohamed Salim (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Tito Mganwa (katikati)

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Lwengera- Darajani, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Korogwe Dkt. Sofia Kabome amesekuwa mwaka wa fedha 2021/2022, halmashauri hiyo ilitenga kiasi cha zaidi ya milioni 23 kupitia mapato ya ndani ikiwa ni agizo la Waziri Mkuu Kasim Majaliwa kuanzisha zahanati kila kijiji na mtaa.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 zaidi ya milioni 65 zilitumika kwa ajili ya umaliziaji ikiwa ni fedha kutoka Serikali Kuu, ambapo utekelezaji wa mradi umejumuisha ujenzi wa engo la agonjwa wa nje (OPD), jengo la mama na mtoto, jengo la mama, baba na mtoto (RCH), kichomea taka, placenta pit na vyoo matundu manne (4).

“Ujenzi huu umekamilika kwa asilimia 75 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 robo ya pili, halmashauri imepokea milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati fedha hizi zimepokelewa Oktoba 30, 2023 pia milioni 50 zimepokelewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya zahanati,” amesema Dkt. Kabome.

Mjumbe wa NEC Taifa kutoka Mkoa wa Tanga Mohamed Salim (wa tatu kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mgombezi Dkt. Paulo Anyabwile (kushoto) kuhusu mashine saidizi ya mtoto mchanga (Neonatal Resusaction machine) kwa ajili ya kuwaweka sawa watoto wenye changamoto ya upumuaji, joto mwili na ute mwingi mdomoni (secretion)

Dkt. Kabome amesema hadi sasa kiasi cha zaidi ya milioni 89 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo na kwa fedha zilizopokelewa kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati na ununuzi wa vifaa tiba, taratibu za awali za manunuzi na utekelezaji wa mradi unaendelea.

Sehemu ya Zahanati ya Lwengera- Darajani, Kata ya Old Korogwe
MNEC kutoka Mkoa wa Tanga Mohamed Salim (wa pili kushoto) akiwa kwenye kikao cha majumuisho Halmashauri ya Mji Korogwe