April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yaridhishwa na utendaji mzuri Tunduma

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetoa rai kwa wakurugenzi wa halmashauri, miji, majiji na manispaa nchini kuhakikisha fedha za serikali zinazotolewa kwa lengo la kutekeleza miradi inayolenga kuimarisha huduma za wananchi, zisiwe zinakaa muda mrefu kwenye akaunti badala yake utekelezaji uwe wa haraka na ubora unaotakiwa ili wananchi waanze kunufaika kwa wakati.

Akizungumza hayo, Katibu wa Halamshauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi ,Shaka Hamdu Shaka, mara baada kukagua ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri ya mji wa Tunduma na ujenzi wa kituo cha chipaka ikiwa ni ukaguzi wa miradi ya utekelezaji wa ilani ya Chama chao.

Amesema, zipo baadhi ya Halmashauri za miji, majiji na manispaa nchini zinazo fursa na vyanzo vizuri vya kukusanya mapato lakini kukosekana kwa ubunifu, uadilifu na ushirikiano baina ya mkurugenzi, wataalam, madiwani na kamati za ulinzi na usalama, wameishia kukusanya chini ya kiwango na kutaka kutegemea serikali kuu kwa kila kitu.

Shaka amepongeza juhudi zinazochukuliwa na halmshauri ya Tunduma katika kusimamia matumizi ya fedha na kutatua kero za wananchi, kuimarisha huduma za kijamii na kujitahidi kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uweledi, uaminifu na ungalifu mkubwa hasa fedha za serikali kuu.

“Halmashauri ya mji wa Tunduma ni mfano mzuri wa kuigwa, Rais Samia mnamtendea haki katika eneo hili nimpongeze Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji,Regina Bieda, Wataalam wake, Madiwani na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Momba kwa namna wanavyosimania ukusanyaji mzuri wa mapato ya Serikali pamoja na matumizi” amesema Shaka

Wakati huo huo,Shaka amekutana na Mwenyekiti wa shina namba 1 Kata ya Chapwa Jimbo la Tunduma pamoja na wanachama wa Chama hicho,na kuwaeleza madhumuni ya ziara yao ikiwa ni kuendelea kuimarisha uhai wa Chama na kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025,kusikiliza na kupokea kero za wananchi kwa ajili ya kutatua changamoto zake .

“Nawashukuru wananchi wa Tunduma kwa kuiamini CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwachagua madiwani wote, Mbunge na Rais kwa ushindi wa kishindo,imani yenu kwa CCM tutailinda, tutaitunza na tutaipa thamani kwa kuwaletea maendeleo ya kweli na kuimarisha huduma kwenu,”amesema

Aidha amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Tunduma, Madiwani na Wataalam wake kwa ukusanyaji mzuri wa mapato huku akisisitiza ongezeko la makusanyo liendelee kuonekane kwa wananchi kwa kuimarisha huduma na kuwajengea mazingira mazuri ya kiuchumi.