April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM na CPC kuendeleza mahusiano yao na kudumisha urafiki

Na Mwandishi wetu, timesmajira.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,Daniel Chongolo amesema kuwa, kupitia dhamana ya kuongoza Serikali na nchi, Chama chao kitahakikisha urafiki wa muda mrefu kati yao na na Chama cha Kikomunisti cha Cuba (CPC).

Pia amesema uhusiano wa Tanzania na Cuba unaendelea kuimarika zaidi, kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya watu wa pande hizo mbili, kupitia ushirikiano imara kwenye nyanja za kilimo, afya na elimu.

Katibu Mkuu Chongolo ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Novemba 2, 2022, wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Ndugu Yordenis Despaigne Vera, wakati balozi huyo alipofika kumtembelea Ndugu Chongolo, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es salaam.

Katibu Mkuu Chongolo amefafanua kuwa, Tanzania na Cuba kupitia vyama vya CCM na CPC kwa miaka 60 sasa, vimekuwa na ushirikiano na urafiki wa kihistoria, ulioasisiwa tangu wakati wa viongozi waasisi wa mataifa hayo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Fidel Castro katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Amesema hata hivyo viongozi wa sasa, kupitia vyama na serikali hizo, wanao wajibu mkubwa wa kuimarisha zaidi na kuuendeleza kwa ajili ya tija na ustawi kwa jamii za nchi hizo.

Kwa upande wake, Balozi Yordenis Despaigne Vera ameeleza kuwa ni muhimu na lazima, kwa pande hizo mbili kuendelea kufanya kufanya kazi kwa pamoja zaidi ili kuendeleza uhusiano na urafiki ulioanzishwa na waasisi hao na kujengewa misingi imara kwa miaka kupitia vyama vya CCM na CPC.