Yawataka wasiondoke eneo hilo, yajipanga kumvaa DC, Kamati ya Siasa ya Wilaya, wenyewe wajivunia zindiko la mganga wao
Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
BAADHI ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kawe, wamebainika kuwa kikwazo cha kuondoka kwa wakazi wa eneo la Kijijini lililopo Mtaa wa Mbezi Beach B, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kama ilivyoamuliwa na Serikali wilayani Kinondoni.
Wakazi hao wa eneo la Kijijini ambako zinaishi kaya kati ya 30 hadi 40, wanatakiwa kuondoka eneo hilo baada ya kujihalalishia vitendo vya uhalifu hadharani, ikiwemo uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, matumizi ya pombe haramu ya gongo na ngono za nipe nikupe.
Pamoja na wakazi hao kupewa siku 14 za kuondoka eneo hilo, ambazo zimemalizika wiki iliyopita, imebainika kwamba miongoni mwa wanaowatia kiburi ni baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Kawe, ambapo mmoja wao anaendesha biashara ya Pool Table eneo hilo.
Katika mkutano uliofanyika juzi baina yao na baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Kawe, wakazi hao walitakiwa kutoondoka eneo hilo hadi Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Kawe itakapokutana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kinondoni ili kutatua tatizo hilo.
Maelekezo hayo yaliyotolewa na kiongozi huyo wa CCM Kata ya Kawe kuwataka wasiondoke, yametafsiriwa na wakazi hao kama ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na mganga kutoka mkoani Mtwara, aliyeletwa na baadhi ya wananchi hao kwa ajili ya kuwafanyia zindiko ili wasiondoke wala kubugudhiwa.
“Kwa kweli ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya viongozi wa CCM Kata wanapingana na viongozi wa Serikali, huku ni kuwapa kiburi, CCM haijivunii wapiga kura wanaojihusisha na uhalifu,” amesema mmoja wa watoa habari wetu aliyehudhuria mkutano huo wa juzi.
Kibaya zaidi Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mbezi Beach B amepewa maelekezo ya kutowabugudhi wakazi hao, kauli ambayo inazidi kuonekana ni matokeo ya kazi iliyofanywa na mganga aliyewasili tangu Jumapili usiku na kuanza kazi yake.
Katibu wa CCM Kata ya Kawe, Aisha Katundu, akizungumza na gazeti hili jana, alisema mara baada ya kupokea kero za wanachama wa kata ya Kawe eneo la Kijijini kwamba walipewa notisi ya siku 14 na Mkuu wa Wilaya kuondoka eneo hilo, waliomba kwa uongozi wa CCM waongezewe muda.
Alisema waliomba wapewe muda kutokana na baadhi yao kuwa na vijana waliokuwa wakisoma na wamefanya mitihani ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili na cha nne, hivyo wanahitaji kusubiria matokeo yao wakiwa kwenye makazi yao eneo hilo.
“Kwa hiyo sisi kama Chama tulipokea ombi lao na tunalifanyia kazi ikiwemo kuwa na mipango ya kwenda kuzungumza na mkuu wa wilaya ya Kindondoni kuhusiana na ombi lao,” amesema Katundu.
Naye Mwenyekiti wa Kata ya Kawe, Othman Chipeta alisema waliongea na wakazi wa Kijijini na sasa watakwenda kuwasilisha ombi lao kwa DC kwa sababu eneo hilo wapo pia wana-CCM.
Hata hivyo, alikiri kuwa wapo wanaovuta dawa za kulevya, lakini pia wapo watu wazuri kwa hiyo Mkuu wa Wilaya ndiye mwenye maamuzi.
Katibu Mwenezi Kata ya Kawe, Yasufu Ndanga (Potipoti) alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu CCM Kata ya Kawe kuwazuia wasiondoke eneo hilo, alijibu; “Siwezi kuongea kwenye simu suala hilo.”
More Stories
Dk Mwinyi ameifungua Skuli Kisiwani Tumbatu yagharimu Sh. Bii 7
Kyobya: Watakaohusika kudhoofisha jitihada za Serikali,Pori la Akiba Kilombero kushughulikiwa
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana