May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Kata 14 yatakiwa kuongeza idadi ya wanachama

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Kata 14 wilayani Temeke kimetakiwa kuongeza idadi ya wanachama wa chama hicho ili kiwe na nguvu zaidi katika chaguzi mbalimbali.

Katika kuazimisha miaka 47 ya chama hicho kimeazimia kuanzia shina hadi Taifa idadi ya wanachama wanaongezeka, lengo ni kuimarisha uhai wa chama.

Akizungumza na Wanachama wa CCM Kata 14 Februari 3, 2024, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Temeke, Happy Nasilika Nyema amesema ili chama kiwe na nguvu lazima kuwepo na idadi kubwa ya Wanachama.

Amesema, ipo idadi kubwa ya wakazi wa kata ya temeke si wanachama wa chama hicho, hivyo ameitaka kata hiyo kuishawishi idadi hiyo iweze kujiunga na CCM.

Happy amepewa idadi ya wanachama wa kata ya Temeke na Katibu Kata wa kata hiyo, Mzee Kiame kuwa, Wanachama wapo 2371 kati ya hao wanaume 1136 na wanawake 1235, huku kukiwa na wakazi 21732.

Amesema, kutokana na idadi ya wanachama ukilinganisha na idadi ya wakazi wa Kata hiyo hailingani kwani takribani wakazi 18,000 hawana chama.

“Ndugu zangu uchaguzi ni namba, hivyo nawaombeni mkawashawishi hawa 18,000 waweze kujiunga na CCM, ili tuweze kuwa na idadi kubwa ya wanachama iwapo chama chetu kinahitaji ushindi katika chaguzi zijazo,” amesema Happy.

Happy amesema, Chama cha Mapinduzi pia kina jumuiya tatu, Jumuiya ya Vijana, Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania, kwa hiyo alizitaka jumuiya hizo nazo ziongeze idadi ya wanachama.

“Natamani jumuiya hizi nazo ziwe na wanachama 2371 kila mmoja kama ilivyokuwa kwenye kata, ili CCM iwe na nguvu zaidi na tuweze kushinda kwa kishindo,” amesema.

Katika hatua nyingine, mjumbe huyo wa Kamati ya Siasa Wilaya aliwakumbusha wanachama wa CCM Kata 14 kulipa ada kwani ndio mtaji mkubwa wa chama.

Amesema, Ada inafanya kazi mbalimbali za Chama hasa katika kukiimarisha pamoja na kuwapa motisha mabalozi wa mashina.

Hata hivyo, amewakumbusha viongozi kuwa wawe wanakaa vikao kila mara kuanzia shina hadi kata kwani ndio vinajenga uimara wa chama.

Lakini pia amesema, anatamani uchaguzi ujao wa wenyeviti wa serikali ya mtaa mwaka huu Chama Cha Mapinduzi kinashinda ushindi wa kishindo.

Naye Mwenyekiti wa CCM, Kata 14 Jery Koto amesema, wamepokea kwa unyenyekevu walichoambiwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya, hivyo watayafanyia kazi ili kuimarisha chama chao.

Hata hivyo amewataka makatibu kata kutokuwa na ukiritimba wa kung’ang’ania kadi au kuwapa watu wanaowafahamu tu.

Amesema, Makatibu kata wanatakiwa wawape kadi mabalozi wa shina ili wahamasishe kupata wanachama kwa wingi kuliko kukaa nazo ofisini.