Na Mwandishi wetu
WALIMU katika Wilaya za Kilosa mkoani Morogoro na Manyoni mkoani Singida, wameeleza kuwa juhudi za kuwawezesha wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali kuendelea na elimu zimeanza kurejesha matumaini ya kutimiza ndoto zao.
Wanasema elimu ni daraja muhimu linalomwezesha mtoto kuvuka kutoka kwenye ndoto na kufikia maisha anayoyatamani, lakini baadhi ya watoto, hususan wa kike hukatisha safari hiyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito, ndoa za utotoni, umaskini na mazingira magumu ya kifamilia.

Kwa mujibu wa walimu hao, baadhi ya wanafunzi waliokatisha masomo wamepata nafasi ya kurejea shuleni kupitia programu zinazolenga kuwasaidia watoto walio katika mazingira magumu, huku wengine wakipata fursa ya kuendelea na elimu ya ufundi na vyuo vya kati na vya juu.
Ofisa Elimu Taaluma Sekondari wa Wilaya ya Kilosa, Milandu Kinyonga anasema,Shirika la CAMFED kwa sasa linafadhili shule 34 kati ya shule 56 zilizopo wilayani humo.
Anasema halmashauri imeendelea kuomba shirika hilo kuongeza wigo wa ufadhili ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wenye mahitaji.
“Wakimaliza kidato cha nne, hatutaki wakae tu bila kufanya shughuli yoyote, ndio sababu tunawapa elimu ya afya ya uzazi pamoja na ujasiriamali ili waweze kufanya shughuli ndogo ndogo za kuwaingizia kipato wanapokuwa nyumbani,” anasema Kinyonga.
Anasema baadhi ya wanafunzi wanawezeshwa kuanzisha biashara, huku wengine wakifanya shughuli za kilimo, ikiwamo kilimo cha matikiti maji.
Kinyonga anasema,CAMFED pia imekuwa ikiboresha mazingira ya kujifunzia kwa kusaidia shule zinazokabiliwa na changamoto za malazi.
Anasema baadhi ya shule zimepatiwa vitanda 20 na magodoro 40 kwa ajili ya wanafunzi wanaolazimika kulala shuleni.
“CAMFED imewezesha pia vitu mbalimbali kwa wanafunzi hawa, ndio sababu wamekuwa na hatua kubwa kimasomo na yapo mafanikio makubwa yanaonekana.Hizi ni juhudi za shirika hili kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa,”anasema Kinyonga.
Wanafunzi wafikia vyuo
Kinyonga anasema, juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda, ambapo baadhi ya wanafunzi waliokuwa katika mazingira magumu wameweza kuendelea hadi kidato cha tano na sita, vyuo vya kati na vyuo vikuu.
Anaeleza kuwa baadhi ya mabinti wana majukumu makubwa ya kifamilia , hivyo kuhitaji msaada wa kielimu na kijamii ili waweze kuendelea na masomo.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Wilaya ya Kilosa, Sebastian Msuya anasema, CAMFED imekuwa mdau muhimu katika sekta ya elimu kwa kusaidia miradi mbalimbali inayolenga kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo.
Msuya anasema,baadhi ya shule zilizopata maboresho ya vifaa vya malazi ni Mazinyungu na Gongwe, huku wanafunzi wengine wakisaidiwa fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu ya shule.
Hata hivyo anasema wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali pia wamekuwa wakisaidiwa baiskeli ili kurahisisha usafiri wa kwenda na kurudi shuleni.
“Tumekuwa tukifanya juhudi kubwa kwa kushirikiana na Halmashauri na CAMFED kuwarejesha shuleni. Mtoto akipata changamoto ya kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito, baada ya kujifungua anarejeshwa shuleni na kufuatiliwa ili kuona mwenendo wake wa masomo,” anasema Msuya.
Anasema pia Halmashauri, CAMFED na wadau wengine wa elimu wamekuwa wakifanya vikao vya tathmini ili kufuatilia utekelezaji wa miradi, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za elimu.
Msuya anasema,jitihada za CAMFED katika kuwafuatilia wanafunzi waliokatisha masomo zimekuwa muhimu katika kuwasaidia kurejea kwenye mfumo wa elimu na kufikia malengo yao.
Mazinyungu yawapa nafasi waliokatisha masomo
Mwalimu wa Stadi za Maisha katika Kituo cha Mazinyungu cha mfumo usio rasmi kwa wanafunzi waliokatisha masomo, Ruth Chahiwa anasema, kituo hicho kinatoa elimu kwa watoto waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali.
Anasema mwaka 2024 wanafunzi sita walifadhiliwa na CAMFED, huku mwaka 2025 wengine sita walisajiliwa na kufanya jumla ya wanafunzi 12 kunufaika.
Chahiwa anasema,wanafunzi hao wameonyesha mafanikio makubwa baada ya kufanya mitihani ya kidato cha nne, huku baadhi yao wakifanikiwa kuendelea na masomo katika vyuo vya kati na vyuo vikuu.
“CAMFED imewasaidia katika mazingira mbalimbali, ikiwamo kuwapatia mahitaji muhimu ya shule kama mabegi, viatu na madaftari. Wanaotoka umbali mrefu pia hununuliwa baiskeli,” anasema.
Anasema msaada huo umewapa wanafunzi ujasiri wa kusoma na kufanya vizuri kwa kuwa changamoto za mahitaji ya shule zimepungua.
Manyoni: CAMFED imewapa wanafunzi kiu ya kusoma
Kwa upande wa Wilaya ya Manyoni, Mwalimu Mlezi wa CAMFED, Beatrice Mwanga anasema,shirika hilo limekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi waliokatisha masomo na wale wanaotoka katika mazingira magumu.
Anasema kwa kipindi cha miaka mitatu, wamekuwa wakiwasaidia wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne, lakini mahitaji bado ni makubwa.

“Ombi letu ni tusaidiwe kuchukua hata wanafunzi wa madarasa ya chini waweze kufadhiliwa, kwani uhitaji ni mkubwa.CAMFED imetufanyia mambo makubwa sana. Asilimia kubwa ya wanafunzi wanashukuru kwa ufadhili wanaoupata kwa sababu umewafanya wawe na kiu ya kusoma,” anasema Mwanga.
Anasema uwezeshaji huo umeendelea kuwapa wanafunzi nafasi ya kurejea kwenye mfumo wa elimu, kujiamini na kujenga msingi wa maisha yao ya baadaye.
Kwa walimu hao, kuwasaidia wanafunzi waliokatisha masomo si suala la kuwarejesha tu darasani, bali ni kuwarudishia matumaini na kuwapa nafasi nyingine ya kutimiza ndoto zao za kielimu na maisha.

More Stories
Umuhimu wa Serikali,Sekta Binafsi kuchochea uchumi wa Tanzania
Kurudi Shuleni baada ya Ujauzito,Safari yenye Miiba
Mkonge wageuka fursa mpya kwa wakulima,AMCOS zakabidhiwa viwanda