November 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Namna AFERA-ARMFA ilivyopitisha Azimio la Nairobi ili kuimarisha miundombinu 

Na Judith Ferdinand 

BARABARA ni kiungo muhimu katika kukuza biashara, kuunganisha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi, lakini ili ziendelee kutoa huduma kwa muda mrefu, zinahitaji mifumo imara na endelevu ya ufadhili wa matengenezo.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (AFERA-ARMFA) kimepitisha Azimio la Nairobi kuhusu Mifuko ya Barabara ya Kizazi Kijacho, hatua inayolenga kuleta mageuzi katika ugharamiaji na usimamizi wa miundombinu ya barabara barani humo.

Rais wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo Barabara Afrika (ARMFA) na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Tanzania, Mha. Rashid Kalimbaga akizungumza wakati akifunga mkutano Mkuu wa 23 wa Mwaka wa chama hicho uliofanyika jijini Nairobi nchini Kenya

Azimio hilo limepitishwa wakati wa kuhitimisha Mkutano Mkuu wa 23 wa Mwaka wa chama hicho uliofanyika jijini Nairobi nchini Kenya, uliowakutanisha wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wakuu wa mifuko ya barabara, mawaziri na wadau wa maendeleo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano huo, Rais wa AFERA-ARMFA na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania, Mhandisi Rashid Kalimbaga anasema,wakati umefika wa kubadilisha mijadala na tafiti zilizofanyika kuwa maamuzi ya kihistoria na utekelezaji wa vitendo.

“Katika siku hizi chache tumefanya kazi kubwa ya kujadili matumizi ya teknolojia (digitalisation), ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na utawala bora wa shoroba za usafirishaji. Leo tumepiga hatua muhimu ya kugeuza kazi hiyo kuwa maamuzi thabiti,” anasema Mha. Kalimbaga.

NGUZO KUU ZA AZIMIO LA NAIROBI 

Kwa mujibu wa Mha.Kalimbaga, Azimio hilo linazifunga nchi wanachama katika misingi mikuu yenye lengo la kuhakikisha uendelevu wa mifuko hiyo, ikiwemo kuwa na vyanzo vya mapato ya moja kwa moja, yanayotabirika na yanayoweza kuhimili mabadiliko ya nishati duniani.

Misingi mingine iliyopitishwa ni pamoja na kuwa na bodi zenye uwiano mzuri wa kiutendaji, kufanya maamuzi yanayozingatia takwimu sahihi, kutenga mifuko ya dharura kwa ajili ya majanga, kuingia mikataba ya utendaji kazi (performance agreements), kuongeza uwajibikaji kwa watumiaji wa barabara pamoja na usimamizi wa pamoja wa shoroba za kikanda.

Aidha, Azimio hilo limeweka ukomo wa muda ambapo kila mfuko mwanachama unatakiwa kuandaa mpango kazi wa kitaifa ndani ya kipindi cha miezi 12, huku tathmini ya utekelezaji wake ikifanyika katika Mkutano Mkuu ujao.

VIPAUMBELE  VITANO VYA MAJUKUMU 

Akizungumzia vipaumbele vya utekelezaji wa majukumu yake ya uongozi wa miaka miwili, Mha.Kalimbaga anasisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya uhakika, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za matengenezo ya barabara.

Pia kuhakikisha upatikanaji wa fedha za uhakika kwa ajili ya matengenezo ya barabara, kuimarisha uhuru wa kiutendaji wa Mifuko ya Barabara, kujenga uwezo wa kitaasisi, kuimarisha ushirikiano na ubunifu katika maeneo mbalimbali ya Afrika pamoja na kuongeza ushawishi na mwonekano wa ARMFA katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Anasema mifumo ya ufadhili inapaswa kuwa imara na inayoweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mabadiliko ya mapato yatokanayo na watumiaji wa barabara.

Pia anasema,ni muhimu kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, ufadhili wa tabianchi na mikataba inayozingatia matokeo.

KATIKA KUIMARISHA UHURU WA MIFUKO YA BARABARA 

Mha.Kalimbaga anasema,mifuko hiyo inapaswa kuwa na uhuru wa usimamizi, rasilimali zinazotengwa kwa matumizi yaliyokusudiwa na mifumo imara ya uwajibikaji ili kujenga imani kwa watumiaji wa barabara na wadau wa maendeleo.

ARMFA YAPOKEA PROGRAMU YA EV

Mabadiliko ya nishati duniani pia yamekuwa sehemu ya mjadala wa mkutano huo, ambapo ongezeko la matumizi ya magari ya umeme barani Afrika linatarajiwa kuleta changamoto katika upatikanaji wa fedha za matengenezo ya barabara.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, ARMFA imepokea programu maalumu ya kukadiria athari za mabadiliko hayo na kubaini njia mbadala za kulinda mapato ya matengenezo ya barabara.

Programu hiyo inayojulikana kama Electric Vehicle (EV) Impact Simulator, imetengenezwa kwa msaada wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (UNECA), ikiwa na uwezo wa kukadiria mapato yatakayopungua kadri watumiaji wa magari wanavyohama kutoka matumizi ya petroli na dizeli kwenda kwenye magari yanayotumia umeme.

Aidha, programu hiyo ina uwezo wa kujaribu sera na mbinu mbalimbali za mbadala zinazoweza kutumika kurejesha mapato hayo mwaka hadi mwaka kwa kipindi kinachochaguliwa.

Matumizi ya programu hiyo na matokeo yaliyopatikana yaliwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa ARMFA, ambapo nchi tatu za majaribio ambazo ni Tanzania, Kenya na Msumbiji zilionesha namna programu hiyo inavyofanya kazi.

Uzoefu wa matumizi ya programu hiyo uliwasilishwa na Mhandisi Dkt.Joshua Mwankunda kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania,anayefafanua namna ya kuchakata takwimu muhimu zinazotumika kukadiria kupungua kwa mapato ya fedha za matengenezo ya barabara pamoja na kufanya majaribio ya sera na mbinu mbadala zinazoweza kujazia upungufu huo.

Baada ya uwasilishaji huo, programu hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa ARMFA na kupokelewa kwa niaba ya wanachama na Mha.Kalimbaga.

Mha. Joshua Mwankunda kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania akiwasilisha mada kuhusu teknolojia ya kukadiria athari za magari ya umeme kwa mapato ya matengenezo ya barabara Afrika katika Mkutano Mkuu 23 wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo Barabara Afrika ARMFA unaofanyika jijini Nairobi Kenya

Hata hivyo upokeaji wa programu hiyo unakuja wakati muafaka kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika ambazo zinashuhudia mabadiliko katika sekta ya usafiri kutokana na ongezeko la matumizi ya magari ya umeme.

Mabadiliko hayo yanatoa umuhimu wa kutafuta mifumo mipya na endelevu ya ukusanyaji wa fedha za matengenezo ya barabara kutoka kwa watumiaji wote, ikihusisha aina zote za nishati inayotumika kuendesha vyombo vya usafiri na usafirishaji.

Kupitia teknolojia hiyo, Tanzania pamoja na nchi wanachama wa ARMFA zitakuwa na nyenzo muhimu ya kusaidia kufanya tathmini na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto za baadaye za upatikanaji wa fedha za matengenezo ya barabara, ili kuhakikisha barabara zinaendelea kutoa huduma endelevu kwa jamii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Sanjari na hayo Mha.Kalimbaga anasema,ARMFA imepiga hatua katika kuanzisha Sekretarieti ya Utendaji, kufanya utafiti wa RRAM kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kuanzisha mafunzo ya awali ya Chuo cha ARMFA, kuunda Kamati ya Kisayansi na kusaini Itifaki ya Ushirikiano na UNECA.

Hata hivyo, anaonya kuwa bado kuna changamoto katika hali ya miundombinu ya barabara barani Afrika, licha ya umuhimu wake katika kukuza biashara na kuunganisha nchi za bara hilo.

Anasema,zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa zinazosafirishwa barani Afrika hutumia barabara, hivyo ubora na uimara wa miundombinu hiyo ni muhimu katika kuimarisha biashara ya ndani ya Afrika, hususani kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), lenye soko la watu takribani bilioni 1.3.

Akitoa mfano wa mafanikio ya Tanzania, Kalimbaga anasema,mapato ya Mfuko wa Barabara hapa nchini yaliongezeka kwa asilimia 45 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2024/25, yakichangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za bandari na usafirishaji wa mizigo ya nchi jirani kupitia Tanzania.

Anasisitiza kuwa ujenzi wa barabara ni mwanzo tu wa uwekezaji katika miundombinu, huku matengenezo yakiwa ndiyo yanayohakikisha barabara zinaendelea kutoa huduma kwa uchumi na wananchi kwa muda mrefu.

Katika mkutano huo,Mha.Kalimbaga anasisitiza umuhimu wa kufikiwa kwa maamuzi mahususi, yakiwemo kupitishwa kwa dira mpya ya ARMFA na mpango kazi wenye gharama za utekelezaji, kuandaliwa kwa Mpango wa Kuboresha Utawala kwa kila Mfuko wa Barabara na kuendelezwa kwa pendekezo la kuanzisha Mfuko wa Dhamana wa Bara la Afrika kwa ajili ya Matengenezo ya Barabara (FFC-ER).

Sanjari na hayo,Mha.Kalimbaga anawahimiza wanachama wote kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za umoja huo kwa uwazi na kulipa ada zao za uanachama kwa wakati ili kuiwezesha sekretarieti kutekeleza mageuzi yanayokusudiwa.

Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Mifuko ya Kizazi Kipya ya Matengenezo ya Barabara: Ufadhili wa Kiwango cha Bara, Muunganiko wa Kikanda na Ustahimilivu kwa Afrika Iliyounganishwa” umewakutanisha wawakilishi wa nchi 35 pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya barabara na maendeleo.

WITO KWA SERIKALI 

Mha.Kalimbaga anatoa wito kwa Serikali, washirika wa maendeleo na wadau wa sekta ya barabara kuendelea kushirikiana katika kuimarisha mifumo endelevu ya ufadhili wa matengenezo ya barabara.Ambapo anaeleza kuwa kutunza barabara ni kulinda uwekezaji wa nchi, kuokoa maisha na kuunganisha masoko na wananchi.

Baadhi ya washiriki waMkutano Mkuu 23 wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo Barabara Afrika ARMFA uliofanyika jijini Nairobi Kenya