November 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Namna minara ya UCSAF ilivyobadili maisha vijijini

Na Judith Ferdinand

KUTEMBEA umbali wa kilomita 15 kutafuta mawasiliano, kushindwa kuuza samaki kwa wakati na kukosa fursa za biashara zinazopatikana kupitia mifumo ya kidijitali ni baadhi ya changamoto ambazo wananchi wa maeneo ya vijijini na visiwani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa walikuwa wakikabiliana nazo kutokana na huduma hafifu za mawasiliano.

Kwa baadhi ya wananchi ilikuwa ili kupata huduma ya mawasiliano iliwalazimu kwenda milimani au nje ya vijiji vyao ili kuwasiliana na ndugu, jamaa na wafanyabiashara wenzao.

Hata hivyo, hali hiyo imeanza kubadilika kufuatia juhudi za Serikali za kupanua huduma za mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambapo kwa Kanda ya Ziwa, jumla ya miradi 20 (ikijumuisha DTP PH1 na PH8) ya kupeleka huduma za mawasiliano ya simu vijijini imetekelezwa na kukamilika tangu kuanzishwa kwa UCSAF.

Ofisi ya UCSAF Kanda ya Ziwa inahudumia mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Shinyanga na Simiyu, yenye jumla ya wilaya 35 na halmashauri 43. Kupitia miradi hiyo, jumla ya minara 414 imejengwa katika kata 326 ambapo kwa Mkoa wa Geita minara 70, Kagera minara 113, Mara 65, Mwanza 61, Shinyanga 44 na Simiyu 61. 

*Mradi wa Mawasiliano ya Simu awamu ya 08 na Mradi wa Tanzania ya Kidijgitali (DTP) 

Kupitia Mradi wa Mawasiliano ya Simu awamu ya 08 na Mradi wa Tanzania ya Kidijgitali (DTP),Serikali kupitia UCSAF iliwezesha na kukamilisha utekelezaji wa ujenzi wa minara 164 katika kata 161 kwa ruzuku ya sh.bilioni 23.6 katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa. Hadi kufikia Desemba 31, 2025, ujenzi wa minara yote 164 katika kata 161 ulikuwa umekamilika na minara hiyo ilikuwa inatoa huduma za mawasiliano.

Kwa Mikoa, Mkoa wa wa Geita ilijengwa minara 19, Kagera minara 45, Mara minara 30, Mwanza minara 18, Shinyanga minara 29 na Simiyu minara 23.

Wananchi katika maeneo yaliyonufaika na mradi huo wanasema kuimarika kwa mawasiliano kumewasaidia kuanzisha biashara, kuongeza kipato, kurahisisha miamala ya kifedha na kupata fursa za kidijitali, huku wavuvi wakieleza kuwa huduma hiyo imewasaidia kupunguza hasara inayotokana na kuchelewa kuuza samaki.

Taarifa ya UCSAF Kanda ya Ziwa iliyotolewa Agosti 10,2026 na Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa UCSAF Fredy Kandonga katika mafunzo ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Mwanza inaeleza zaidi kuwa Serikali kupitia UCSAF inatekeleza mradi mpya wa kufikisha mawasiliano ya simu katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa kupitia Mradi wa Mawasiliano ya Simu Awamu ya 10 ambao unahusisja ujenzi wa minara 80 katika kata 79 za Mikoa sita ya Kanda ya Ziwa.

 Kupitia mradi  huo utahusika ujenzi wa minara 24 kwa Mkoa wa Mwanza, Kagera minara 16, Mara minara 13, Simiyu minara 11, Shinyanga minara tisa na Geita minara saba. 

Mradi huu unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kuhudumia wakazi takribani 965,925 walioko katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa kwa gharama ya sh. bilioni 7.925. Utekelezaji wa Mradi umepangwa kuchukua miezi 15 kuanzia Desemba 5, 2025. 

Mradi huo pia utawezesha ujenzi wa minara kwenye visiwa vya Rukuba Kata ya Etaro Musoma na Katunguru kisiwa cha Juma Sengerema. Mpaka sasa tayari ujenzi wa minara 34 kati ya 80 inayotarajiwa kujengwa katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa umekamilika na inatoa huduma kwenye maeneo yaliyolengwa.

 Minara hiyo iliyowaka ni ile ya Geita (Butinzya, Butengorumasa, Nyijundu); Kagera (Kasulo, Lusahunga, Nyakato, Biirabo,Kibimba,Kibogora, Muganza, Nyamiyaga); Mara (Musanja, Itiryo); Mwanza (Nyakasasa, Fella, Luchelele, Murutunguru, Mantare, Mwankulwe, Ilujamate, Mwaniko, Sumbugu, Nyamatongo); Shinyanga (Ikinda, Mega, Ngaya, Nyankende) na Simiyu (Mbaragane, Ipililo, Ikindilo, Isanga, Zanzui, Mwamishali, Mwandoya).

Hata hivyo  kuwaka kwa minara hiyo kumeongeza idadi ya minara iliyojengwa na Serikali kwa ruzuku yake kupitia UCSAF kufikia 448 mpaka sasa huku ukekelezaji ukiendelea kwenye maeneo yaliyobaki. .

Mbali na minara iliyojengwa nchi kavu pia Serikali kupitia UCSAF imewezesha ujenzi wa minara visiwani ikiwemo Kata ya Ilangala Kisiwa cha Gana Ukerewe, Kata ya Chifunfu kisiwa cha Lyakanyasi Sengerema, Kata ya Kahangara Kisiwa cha Ijinga Magu na Kata ya Kerebe Kisiwa cha Makibwa Muleba. 

Aidha UCSAF Kanda ya Ziwa imesimamia ujenzi wa minara mitatu ndani ya Ziwa Victoria kupitia mradi wa kuimarisha usalama unaotekelezwa na Mamlaka ya Usafiri wa Majini Tanzania (TASAC), kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. 

Minara hiyo iliyojengwa na TTCL ipo Kagunguli (Kisiwa cha Kweru) na Bwiro (Kisiwa cha Kunene), Wilaya ya Ukerewe, na mnara wa Bulyaheke (Kisiwa cha Soswa), Wilaya ya Sengerema ambayo yote imekamilika na inatoa huduma. .

Katika kuendelea kuimarisha mawasiliano na usalama ndani ya Ziwa Victoria, Serikali kupitia UCSAF imepanga kujenga minara mingine miwili katika maeneo ya Bukindo na Nabweko, Lyegoba, Wilaya ya Ukerewe.

Hata hivyo, utekelezaji wa miradi hiyo unakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo usafirishaji wa vifaa vizito katika maeneo ya visiwani kutokana na ukosefu wa miundombinu inayofaa, pamoja na mawimbi makubwa ya Ziwa Victoria yanayofanya usafirishaji kuwa mgumu. 

Changamoto nyingine ni ukosefu wa barabara katika baadhi ya maeneo yaliyopangwa kujengwa minara na ucheleweshaji wa vibali kutoka baadhi ya mamlaka na taasisi za Serikali. UCSAF Kanda ya Ziwa imeahidi kuendelea kusimamia miradi ambayo haijakamilika na kushirikiana na watoa huduma, wakandarasi,Wakurugenzi wa Halmashauri na taasisi nyingine za Serikali kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.

*Mawasiliano yabadilisha maisha Chato

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kikumbataile Kata ya Kigongo, Wilaya ya Chato mkoani Geita, Alphonce Gombokile anasema, wananchi wamekuwa na changamoto ya mawasiliano kwa muda mrefu, lakini changamoto hiyo imeisha baada ya Serikali kuwezesha ujenzi wa mnara kijijini hapo.

Anasema,walipata taarifa za uwepo wa mradi huo walipohudhuria kikao kimoja wilayani, ambako waliambiwa kuwa Serikali kupitia UCSAF ilikuwa imewezesha ujenzi wa minara minne katika Wilaya ya Chato, huku Kata yao ikinufaika na mnara mmoja.

“Tunashukuru Serikali kwa kuwezesha mawasiliano, kwani hapo awali tulikuwa na changamoto kubwa kutokana na mawasiliano kuwa hafifu sana,” anasema Gombokile.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kikumbataile, Boniface Clement anasema, mnara huo umefungua fursa za biashara na ajira kwa vijana, ambao baadhi yao wameanzisha biashara za kutoa huduma ya intaneti kupitia Wi-Fi ili kuongeza kipato. 

Anasema kuimarika kwa mawasiliano kumewezesha kuongezeka kwa huduma za kifedha, zikiwemo M-Pesa na Airtel Money, huku wananchi wakianza kutumia mifumo ya kidijitali katika kufanya miamala na kuhifadhi fedha.

Clement anaeleza kuwa vikundi vya kijamii vimeanza kutumia huduma za kidijitali, ikiwemo M-Koba, kuhifadhi fedha zao, hatua inayosaidia kurahisisha shughuli zao za kifedha na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na kutunza fedha taslimu nyumbani.

“Kwa hiyo, tunashukuru Serikali na UCSAF kwa kutuletea huduma hii. Kijiji chetu kimeanza kupiga hatua, kwani hapo awali tulikuwa tunakabiliwa na changamoto kubwa na tulishindwa kufanya biashara kwa urahisi,” anasema.

Wavuvi wapunguza hasara

Mkazi wa Kijiji cha Kikumbataile, Alphonce Binna anasema, kukosekana kwa mawasiliano kulikuwa changamoto kubwa kwa wavuvi, hasa katika kuratibu shughuli zao na kutafuta wanunuzi wa samaki.

Anasema kulikuwa na tukio la mtu mmoja kushambuliwa na mamba na kufariki dunia kutokana na kukosekana kwa mawasiliano, hali iliyodhihirisha umuhimu wa huduma hiyo katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.

Binna anaeleza kuwa kabla ya kuimarika kwa mawasiliano, wavuvi walikuwa wakipata hasara kutokana na kuchelewa kuuza samaki waliovuliwa, huku bei zikishuka kwa sababu ya kukosa wanunuzi kwa wakati.

“Tulikuwa tukivua samaki, lakini kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano, samaki walikuwa wakiharibika kwa kuchelewa kuuzwa, hivyo mvuvi aliingia hasara. Samaki ambao walipaswa kuuzwa kwa sh. 10,000/- kwa kilo tulijikuta tunawauza kwa sh.5,000 hadi sh.1,000,” anasema Binna.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Joyce Malikusi anasema, awali wananchi walilazimika kutafuta maeneo yenye mtandao, ikiwemo kwenda milimani au nje ya kijiji ili kuweza kuwasiliana na watu wengine.

Anasema, hali hiyo ilikuwa ngumu kwa sababu mtu aliyekuwa akitafuta mawasiliano ndiye aliyelazimika kwenda kutafuta mtandao, huku mtu mwingine akishindwa kumpata kwa urahisi.

“Zamani, ukitaka kuzungumza na mtu ilibidi umtafute mwenyewe kwa kwenda milimani au nje ya kijiji. Kama hakumtafuta wewe, ilikuwa vigumu kukupata. Lakini baada ya UCSAF kutuletea mnara, sasa ni kicheko tu,” anasema Malikusi.

*Minara yarahisisha biashara Kagera

Mkazi wa Kyerwa mkoani Kagera, Athuman John anasema,kabla ya kuimarika kwa mawasiliano, wananchi walilazimika kutembea umbali wa kilomita 15 kutafuta mtandao, lakini wakati mwingine walifika walikokusudia na kumkosa mtu waliyekuwa wanataka kuwasiliana naye.

Anasema changamoto hiyo iliongezwa na mwingiliano wa mawasiliano kutoka nchi jirani kutokana na eneo hilo kuwa mpakani, hali iliyofanya wakati mwingine mtu asipatikane kwenye simu.

Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Makibwa Kisiwa cha Kerebe Wilaya ya Muleba Kaskazini mkoani Kagera, Edina Laurent anasema, kuimarika kwa mawasiliano kumewasaidia wananchi kupata mtandao wa simu katika maeneo mengi ya kisiwa hicho.

Laurent, ambaye ni mfanyabiashara, anasema,sasa anaweza kuratibu ununuzi na usafirishaji wa bidhaa kwa kutumia simu na kufanya malipo kupitia M-Pesa bila kulazimika kusafiri kila anapohitaji bidhaa kutoka ng’ambo ya kisiwa hicho.

Anasema kutokana na changamoto za usafiri wa boti, wakati mwingine mfanyabiashara anaweza kukosa usafiri siku aliyopanga, jambo ambalo hapo awali lingeweza kuchelewesha shughuli zake.

Hata hivyo anasema,kuimarika kwa mtandao kumemwezesha kuwasiliana na watu wanaomkusanyia bidhaa na kupanga malipo hata kama hana fedha wakati huo, kisha kutuma fedha siku inayofuata.

Anasema hali hiyo imekuwa kama suluhisho la changamoto za usafiri, kwa kuwa sasa anaweza kuendelea na biashara huku akiratibu upatikanaji wa bidhaa kwa njia ya simu.

Naye mkazi wa Kijiji cha Makibwa, Jamila Masoud, ambaye ni mjasiriamali wa samaki waliokaushwa kwa kubanikwa na kuwasafirisha kwa wateja anasema,mawasiliano yaliyoboreshwa yamemwezesha kuendesha biashara yake akiwa kijijini.

Anasema,sasa anaweza kuwasiliana na wateja katika maeneo mbalimbali, kuwatumia samaki na kupokea malipo baada ya bidhaa kuuzwa bila kulazimika kusafiri mwenyewe.

Kwa upande wake, Annuary Mwami, mkazi mwingine wa Kijiji cha Makibwa anasema,kabla ya ujenzi wa mnara upatikanaji wa intaneti ulikuwa mgumu, hali iliyowafanya wananchi, hususani vijana, kushindwa kupata taarifa za fursa zinazotangazwa kupitia mifumo ya kidijitali ya Serikali.

Anasema hali imebadilika baada ya kuimarika kwa mawasiliano, ambapo wananchi sasa wanapata huduma ya intaneti yenye kasi ya 4G.

“Kwa sasa tunapata intaneti yenye kasi ya 4G. Tunashukuru Serikali kwa kutuletea mnara ambao umeimarisha mawasiliano, na UCSAF kwa kuendelea kusimamia mradi huu. Ingawa hapa hatuzidi watu 300, Serikali imeona ni muhimu wananchi wapate huduma ya mawasiliano,” anasema Mwami.