June 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BRELA yatoa elimu wiki Utumishi wa Umma

Na Joyce Kasiki,Dodoma

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewahimiza wananchi na wafanyabiashara kufika katika banda lake kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali, mkoani Dodoma, ili kupata elimu na huduma mbalimbali za usajili wa biashara kwa papo hapo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuph Mwasakafyuka, amesema taasisi hiyo inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwaelimisha kuhusu huduma zinazotolewa na wakala huo.

Amesema BRELA imekuwa ikitoa huduma katika banda lake tangu kuanza kwa maadhimisho hayo na itaendelea hadi Juni 23 mwaka huu, ambapo wananchi wanapata fursa ya kusajili biashara zao na kupata ushauri kuhusu mifumo ya usajili.

“Tunatumia maadhimisho haya kuonesha huduma tunazozitoa ofisini kwa wananchi. Tunatoa elimu pamoja na huduma za usajili wa papo kwa papo kwa wafanyabiashara na wananchi wote wanaohitaji huduma za BRELA,” amesema Mwasakafyuka.

Ameeleza kuwa BRELA inasimamia sheria kuu sita zinazohusisha usajili wa makampuni, usajili wa majina ya biashara, usajili wa alama za biashara (trademark), usajili wa hataza (patent), utoaji wa leseni za viwanda na leseni za biashara za Kundi A.

Kwa mujibu wa afisa huyo, mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa ambapo zaidi ya watu 200 wamefika katika banda hilo kupata huduma mbalimbali tangu kuanza kwa maadhimisho hayo.

“Zaidi ya watu 50 tayari wamefanikiwa kupata vyeti vya usajili wa majina ya biashara kupitia huduma za papo kwa papo zinazotolewa hapa bandarini,” amesema.

Mwasakafyuka amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni baadhi ya waombaji kutumia taarifa zisizo sahihi wakati wa usajili wa awali, hali inayosababisha ugumu wanapotaka kufikia huduma kupitia maboresho ya mfumo mpya wa usajili.

Amefafanua kuwa baadhi ya wananchi husahau anuani za barua pepe au namba za simu walizotumia wakati wa usajili wa mwanzo, jambo linaloathiri upatikanaji wa huduma katika mfumo ulioboreshwa.

Akizungumzia umuhimu wa usajili wa biashara, amesema urasimishaji wa biashara ni hatua muhimu kwa mfanyabiashara anayehitaji kukuza shughuli zake na kupata fursa mbalimbali za kifedha na kibiashara.

“Ukiwa umesajili biashara yako kupitia BRELA unakuwa umetambulika rasmi. Hii inakupa nafasi ya kupata huduma kutoka taasisi nyingine ikiwemo mikopo ya benki na fursa za biashara za kitaifa na kimataifa,” amesema.

Amewahimiza wananchi wa Dodoma na mikoa jirani kutumia fursa ya maonesho hayo kufika katika banda la BRELA kupata elimu, huduma na ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazohusiana na usajili wa biashara.