April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Mfuko wa Barabara yazionya TANROADS,TARURA fedha za matengenezo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Morogoro

Bodi ya Mfuko wa Barabara, imezitaka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha wanatumia fedha za matengenezo ya barabara zinazotolewa na Mfuko wa Barabara kama ilivyoelekezwa.

Akizungumza mkoani Morogoro Aprili 15, 2024 mara baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa Katibu na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga amesema kuwa bodi itahakikisha inazigawa fedha hizo kwa wakati kwa wakala wa barabara ili kusaidia matengenezo ya barabara kufanyika kwa haraka.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mha. Rashid Kalimbaga, akizungumza jambo, wakati wa mkutano wa kwanza wa baraza hilo unaofanyika kwa siku mbili mkoani Morogoro

“Sisi kama bodi jukumu letu kuu ni kuhakikisha mara  tunapopata fedha, tunazigawa kwa TANROADS na TARURA na haifiki siku tatu fedha hizo zinakuwa zimefika kwao,” amesema Mhandisi Kalimbaga.

 Kalimbaga ameongeza kuwa hadi kufikia Machi, 2024 kiasi cha bilioni 110 kimetolewa kwa TANROADS na bilioni 89 kwa TARURA kwa ajili ya matengenezo ya barabara nchi nzima na kusisitiza Bodi inaendelea kutoa fedha kwa kadri inayoletewa kutoka Hazina.

Pia amefafanua kuwa Bodi inaendelea kufuatilia kwa makini kuhakikisha fedha wanazozitoa zinakwenda kuhudumia yale yaliyokusudiwa.

 Kuhusu uanzishwaji wa Baraza hilo, Kalimbaga amesema kuwa watalitumi kuhakikisha wanajadili na kuzifanyia kazi hoja za watumishi pamoja na kuhakikisha motisha na stahiki kwa zao zinapatikana ili kuleta ari na kasi ya utendaji kazi wa Bodi.

Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara linatarajiwa kuzinduliwa wiki ijayo na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ambapo hatua za awali za uzinduzi huo zimefanyika mkoani Morogoro  Aprili 15, 2024 kwa Bodi hiyo kufanya uchaguzi wa Katibu na Wajumbe wa Baraza hilo.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe/ washiriki wa mkutano wa baraza hilo, linalofanyika kwa siku 2 mkoani Morogoro