May 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wafanyabiashara wa madini wa Mkoa wa Geita hivi karibuni alipofanya ziara ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya maendeleo inayofanywa kwa fedha za huduma za jamii (CSR) zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) uliopo mkoani Geita. (Picha na Wizara ya Madini).

Biteko ataka mchango sekta ya madini kutazamwa vinginevyo

Na Nuru Mwasampeta, WM

WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amewataka Watanzania kuutazama mchango wa sekta ya madini kwa namna unavyosaidia kuinua sekta nyingine za uchumi, kwani tayari kwa upande wa kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli sekta hiyo imeonesha mafanikio makubwa.

“Niliwaambia wenzangu wizarani, lazima tuhame sasa kwenye mfumo wa kufurahia kuona mapato yameongezeka kutokana na ukusanyaji wa maduhuli twende kwenye mfumo wa kujiuliza je? Sekta ya madini imechangiaje ukuaji wa sekta nyingine?.

Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu kutoka kulia) na ujumbe alioambatana nao ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel (kulia kwake) wakikagua ujenzi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu kinachojengwa na mwekezaji binafsi mkoani humo. (Picha na Wizara ya Madini).

“Anayelima mchele awe na uhakika wa wanunuzi kwa sababu wachimbaji wapo, anayefuga ng’ombe awe na uhakika wa soko kwa sababu wanunuzi wapo, anayelima nyanya na shughuli nyingine hivyo hivyo, na huo ndio tunaita ufungamanishaji wa uchumi wa madini na sekta nyingine;

Waziri Biteko amebainisha hayo hivi karibuni mkoani Geita alipofanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo inayofanywa kwa fedha za huduma za jamii (CSR) zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya unaoendelea katika soko kuu la dhahabu Geita pamoja na soko la Katundu litakalohusisha biashara za kawaida lililojengwa katika Halmashauri ya Mji wa Geita.

Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel (kulia) na wajumbe walioambatana nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Madini mkoani humo. (Picha na Wizara ya Madini).

Pamoja na kukagua miradi ya maendeleo inayowezeshwa na GGML, Waziri Biteko amezungumza na wafanyabiashara wa madini mkoani humo na kueleza kuwa kutokana na changamoto ya Covid-19, wizara imetoa kipindi cha miezi mitatu kwa wafanyabiashara wa madini kununua madini mahali popote nchini na kuwataka kuzingatia uwepo wa vibali vyote muhimu vinavyoonesha mahali madini hayo yamenunuliwa na yanakopelekwa mara baada ya kuyanunua.

Akitoa taarifa ya sekta,  Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema mwenendo wa biashara ya madini ya dhahabu katika mkoa wake tangu soko la dhahbu kufunguliwa mwezi Machi 2019 hadi Mei 2020 kipindi cha miezi 14 jumla ya kilo 5,320.99 zenye thamani shilingi Bilioni 522.44 zimeuzwa na kuchangia mapato ya serikali kupitia  mrabaha na ada ya ukaguzi kwa jumla ya shilingi bilioni 36.57.

Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wafanyabiashara wa madini wa Mkoa wa Geita lengo ikiwa ni kusikiliza na kujibu hoja mbalimbali walizonazo katika utekelezaji wa majukumu yao. Pamoja naye ni uongozi wote wa Mkoa wa Geita ukiongozwa na Mkuu wa mkoa, Gabriel Robert na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa. (Picha na Wizara ya Madini).

Amesema, ongezeko hilo linaonesha namna sekta ya madini ilivyokuwa na mafanikio makubwa sana kutokana na usimamizi makini na uongozi bora wa wizara, lakini pia utii na utekelezaji wa ushauri na maelekezo yanayotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Aliongeza kuwa, fedha inayopatikana kutokana na makusanyo kwenye sekta ya madini ndiyo inayokwenda kulipa elimu bure, kujenga vituo vya afya, inatumika katika kujenga hospitali za wilaya na mambo mengine mengi yanayotekelezwa na serikali yetu.

Amebainisha kuwa, mkoani Geita kuna ongezeko kubwa la viwanda vya kuchenjua dhahabu  (Illusion Plant) kutoka viwanda 20 vilivyokuwepo awali na kufikia viwanda 39 na kubainisha kuwa hayo ni mageuzi makubwa katika sekta ya madini kwa kuwezesha uwepo wa viwanda vidogovidogo mkoani humo.

Jengo jipya litakalotumiwa na wafanyabiashara wa madini mkoani Geita ambalo lilijengwa kwa fedha za huduma kwa jamii (CSR) zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) na kusimamiwa kwa ushirikiano baina ya mgodi huo na Halimashauri ya Mji wa Geita. (Picha na Wizara ya Madini).