April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 13 zatumika kuboresha miradi ya elimu Kigoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akitoa maelekezo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga kinachojengwa katika Halmashauri ya Kasulu mkoani Kigoma.

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema kwa sasa Serikali ipo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu mkoani Kigoma yenye thamani ya zaidi bilioni 13.

Profesa Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati akikagua miradi hiyo mkoani humo yenye lengo la kuhakikisha elimu bora inapatikana nchini.

Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kasulu, Chuo cha Ualimu Kabanga na jengo la Utawala la shule ya Sekondari Grand vya mkoani Kigoma.

Akizungumzia maendeleo​ ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga mara baada ya kukagua amesema, chuo hicho kinajengewa upya miundombinu yote​ baada ya ile ya awali kuchakaa sana na kushindwa kukarabatiwa ambapo ujenzi huo umegharimu zaidi ya bilioni 10 na utakapokamilika utabadili taswira ya mji huo kwa kuwa majengo yanayojengwa ni ya kisasa na imara ambayo yatadumu kwa muda mrefu.
​
Kuhusu mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala na utengenezaji wa mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Grand, Profesa Ndalichako amesema, umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 534 na utakapokamilika utaongeza morali ya walimu​ kufundisha na kusaidia wanafunzi waliopo katika shule hiyo.
​
Mradi mwingine uliotembelewa ni wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Kasulu ambao upo katika hatua za mwisho ambao umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.97 ambapo jumla ya majengo 15 yatajengwa​ na kitachukua wanafunzi 320 watakaokuwa wakilala chuoni hapo.
​
Waziri Ndalicahko amewataka wananchi wa Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla kutumia fursa ya kuwepo kwa vyuo mbalimbali katika Halmashauri hiyo kujipatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa ama kujiajiri ili kujiletea maendeleo binafsi na ya mkoa wa Kigoma.

Muonekano wa jengo jipya la utawala la shule ya sekondari Granda lililojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia likiwa katika hatua za mwisho za ukamilishwaji

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia​ kwa namna ilivyojikita katika kupanua wigo wa elimu lakini pia katika Wilaya yake kuna maeneo ambayo ni ya wafugaji na watoto hawakuwa wakienda shule lakini kwa sasa zimejengwa shule shikizi katika maeneo hayo ya mbali hivyo kuwezesha watoto kusoma na kuleta matokeo chanya.
​
Kanali Anange amesema, baada ya Serikali kutekeleza Sera ya Elimu bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi, hivyo kupelekea Serikali kupanua​ miundombinu katika ngazi zote za elimu ili kuwezesha fursa za masomo kwa wanafunzi ikiwemo na kuongeza walimu.​

Ameongeza kuwa, ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu itawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu katika mazingira bora.

Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji wa Elimu ya Ualimu (TESP), Ignas Chonya amesema ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Kabanga awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Oktoba 2020 na chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 400 kwa wakati mmoja na kwamba chuo kinatarajiwa kuanza mafunzo mwaka huu.